Na: Lilian Lundo – MAELEZO - SIMIYU
Umoja
wa Walimu na Wazazi (UWW) katika shule za Msingi za Serikali Kata ya
Migato, Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu umetatua kwa kiwango kikubwa
tatizo la watoto wa kike kuacha shule na kwenda kuolewa.
Mratibu
Elimu wa Kata hiyo Bw. Joshua Balomi, aliyasema hayo Mjini Bariadi
alipokuwa akieleza mafanikio yaliyotokana na uanzishwaji wa UWW katika
Shule za Msingi wakati wa semina ya mawasiliano na kushirikishana
jitihada zenye mafanikio kwenye Elimu, inayoendelea Mjini Baridi.
“Mwaka
jana, 2015 kata yangu ilikuwa na wanafunzi wa kike watatu ambao
walikuwa na uwezo mkubwa darasani na walifanikiwa kufanya vizuri katika
mitihani yao ya MOCK, cha kushangaza wanafunzi hao hao walifanya vibaya
katika mitihani yao ya mwisho ya kuhitimu Elimu ya Msingi.” alifafanua
Balomi.
Uchunguzi
ulifanyika na kubainika kwamba wanafunzi hao walirubuniwa na wazazi wao
wafanye vibaya katika mitihani yao ya mwisho ili wasiendelee na masomo
badala yake waende kuolewa.
Kamati
za UWW zilishirikishwa juu ya tatizo hilo na kuchukua jukumu la kuongea
na wanafunzi wa darasa la saba ambao wamehitimu masomo yao mwaka huu
2016 kwa kuwaambia umuhimu wa elimu na kuwatolea mifano ya wanawake
waliofanikiwa kutokana na elimu waliyoipata.
Aidha
kamati hizo ziliwahusia wanafunzi hao kutokubali kujifelisha ili waende
kuolewa badala yake wazazi wanapowashauri kufanya vibaya katika
mitihani yao ya mwisho kutofuata ushauri huo kwani elimu wanayoipata ni
kwa ajili ya maisha yao wenyewe na sio kwa ajili ya wazazi wao.
Juhudi
hizo za UWW zilizaa matunda ambapo katika matokeo ya darasa la Saba ya
mwaka huu 2016 wanafunzi wote wa kike waliotegemewa kufanya vizuri
katika kata hiyo walifanya vizuri kama ilivyotarajiwa.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment