Na. Lilian Lundo – MAELEZO - Simiyu
Morali
ya ufundishaji wa walimu wa shule ya Msingi Igaganulwa iliyoko kata ya
Dutwa, Halmashauri ya Wilaya ya Baridi Mkoani Simiyu umeongezeka na
kupelekea shule hiyo kuwa na ufulu wa juu wa wahitimu wa darasa la Saba
mwaka 2016.
Mwalimu
Mkuu wa Shule hiyo Robert Majani aliyasema hayo Wilayani Bariadi wakati
wa Mahojiano na timu inayosimamia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu ya
Wilaya hiyo kuhusu maendeleo ya taaluma ya shule yake.
“Miaka
mitatu iliyopita morali ya ufundishaji wa walimu wa shule hii ilikuwa
ya chini kutokana ushirikiano hafifu uliokuwepo kati ya walimu wakuu wa
miaka ya nyuma na walimu wa shule hii, tatizo hilo lilipelekea walimu kuondoka kwenye vituo vya kazi kabla ya muda wa kazi kumalizika pamoja na utoro uliokithili kwa wanafunzi,” alifafanua Mwalimu Majani.
Aliendelea
kwa kusema kuwa, kulikuwa hakuna uwazi wa mapato na matumizi ya fedha
za shule baina ya uongozi wa shule, walimu wa shule hiyo na wadau wa
elimu. Vile vile kulikuwa na upungufu wa vitendea kazi pamoja na samani
za ofisini hivyo walimu kufanya kazi katika mazingira magumu.
Tatizo
hilo la walimu katika shule hiyo lilipelekea ufaulu wa chini pamoja na
utoro uliokithili kwa wanafunzi kutokana na kutokuwepo kwa uangalizi wa
walimu hivyo wanafunzi walikuwa wakienda shule pale wanapopenda.
Katika kurudisha morali ya walimu wa shule hiyo Mwalimu Majani kupitia vikao vya kamati ya taaluma, walimu wakorofi walikoselewa ili kurekebisha tabia, pia kamati ya shule iliunda sungusungu ambao walikuwa wakiwakamata na kuwarudisha shuleni wanafunzi wanaotoroka shule.
Vile
vile walimu walibadilishiwa masomo ya kufundisha baada ya kuonekana
baadhi ya walimu wa masomo ya ufundi kutofanya vizuri katika masomo hayo
hivyo wakapewa masomo ambayo wanayamudu kufundisha.
Mapato
na matumizi ya fedha ya shule hiyo vimewekwa wazi kwa walimu wote
pamoja na kushirikishwa katika upangaji wa bajeti ya shule hiyo.
Aidha
Mwalimu Majani ameanzisha programu ya kutoa chai kwa walimu wa shule
hiyo kwa kutumia posho yake ya madaraka ambapo imesaidia kupunguza muda
wa walimu kwenda kunywa chai mjini ambako ni mbali na shule.
Mabadiliko
hayo yamepelekea kuongezeka kwa hamasa ya walimu kufundisha hivyo
kupandisha ufaulu wa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba ambapo kwa
mwaka 2016 shule hiyo imeshika nafasi ya Sita Kiwilaya kutoka nafasi ya 28 mwaka 2015.
Mwalimu
Majani alisema kuwa sababu nyingine iliyoipelekea shule hiyo kufanya
vizuri zaidi mwaka huu 2016 ni pamoja na mafunzo yanayotolewa na
Serikali kupitia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Nchini (Education
Quality Improvement Programme-Tanzania) EQUIP-T ambapo walimu wamekuwa
wakipata mafunzo ya kuwajengea uwezo ili kuwapa motisha ya kazi.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment