Home » » Zifahamu Sifa za kuwa Mpiga Kura

Zifahamu Sifa za kuwa Mpiga Kura

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



Na Christina Njovu
Vijana mbalimbali mkoani Simiyu wamejitokeza kwa wingi katika banda la Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuweza kupata ufafanuzi juu ya maswala mbalimbali ya Uchaguzi yakiwemo yale yahusuyo Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshiriki katika maadhimisho ya wiki ya vijana katika muendelezo wa ratiba na taratibu iliyojiwekea katika kutoa Elimu ya Mpiga Kura Jukumu ambalo Tume hiyo imepewa kwa mujibu wa Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 74 ya mwaka 1977 kinachoipa mamlaka ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura.
Kwa kutambua umuhimu wa vijana katika kupata elimu ya Mpiga Kura ikiwa ni pamoja na kufahamu kazi mbalimbali za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), pia imelenga kupata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa Uchaguzi juu ya namna ya kuboresha utendaji wake ili chaguzi zijazo ziwe na mafanikio makubwa. 
Ikiwa mkoani Simiyu Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliweza kuwafikia vijana wengi ambapo baadhi ya vijana walihitaji kupata uelewa hasa juu ya sifa za kuwa mpiga Kura ambapo maafisa wa NEC waliweza kutoa ufafanuzi kuwa ili upate sifa za kuwa mpiga kura ni lazima uwe na sifa zifuatazo:-         
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 5 (1) na (2) imaeeleza kuwa sifa za mpiga Kura kuwa ni lazima awe ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa ama kwa kuandikishwa, awe na umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea maana katika umri huo inaaminika kuwa mtu anaacha utoto na kuingia umri wa utu uzima, pia inaaminika kuwa hapo maamuzi unayoyafanya una maanisha kwa maana ni maamuzi sahihi ndipo utapata haki ya kuchaguliwa ama kuachagua kiongozi.
Licha ya kuufikia umri huo wa miaka 18 haitoshi kuitwa Mpiga, ni lazima awe umejiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ni lazima awe na  akili timamu hii ikiwa na maana ya mtu asiwe mgonjwa wa akili kiasi ambao husababisha  kushindwa kutambua nini unachokifanya.
Hali hii ikijitokeza katika baadhi ya maeneo wakati wa zoezi la uandikishaji baadhi ya wanafamilia licha ya kutambua kuwa watoto ama ndugu zao wana matatizo ya akili bado waliwapeleka katika vituo vya kujiandikisha na kutaka wajiandikishe katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2004 kifungu cha 23 (1) kinaeleza kuwa, sifa nyingine za kuwa mpiga Kura ni lazima awe na kadi ya mpiga Kura na jina lake liwemo katika Daftari la Kudumu la wapiga Kura hapo ndipo atapata haki ya kuwa mpiga Kura.
Kwa kuzingatia hilo Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeweka utaratibu maalum ambao unahakikisha kuwa kila mwenye sifa za kuwa mpiga Kura kwa maana ya kufikisha umri wa kupiga kura anapata haki hiyo kwa kuweka vituo vya kupigia Kura katika ngazi ya Kata.
Kuwepo kwa vituo vya Kujiandikishia na hatimaye kupigia Kura katika ngazi ya kata ni kuwezesha wananchi wote wanapata huduma hiyo kwa karibu badala ya kutembea umbali mrefu kupata huduma hiyo.
Wananchi wengi wakiwemo vijana katika maadhimisho hayo ya wiki ya vinjana mkoani Simiyu, waliuliza kuhusu baadhii ya vituo vya kupigia kura kuwepo mbali kiasi cha kufanya baadhi wa wananchi kutembea umbali mrefu kufuata vituo hivyo.
Ni kwamba ili kituo kipate sifa ya kuwa kituo cha kupigia kura ni lazima kiwe na idadi ya wapiga kura wasiozidi  500. Kutokana na jiografia ya nchi yetu, baadhi ya maeneo wananchi wanakaa mbalimbali na hivyo kufanya baadhi yao kutembea umbali mrefu kufuata kituo cha kupigia kura ndani ya kata husika.
Kwa mujibu wa ripoti ya Uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ule wa Serikiali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa  mwaka 2015, idadi ya vituo vya kupigia Kura kwa Tanzania Bara ilikuwa ni vituo 63,525 na vituo 1,580 kwa upande wa Tanzania Zanzibar.
Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2004  kifungu cha 24 (1) kinaeleza kuwa mpiga kura atapiga kura katika kituo alichojiandikishia hii inatokana na sifa ya kuwemo katika daftari la Kupigia Kura ambalo linapatikana katika kituo ulichojiandikishia. 
Eneo hili huzua maswali mengi wakati wa uchaguzi mkuu kwani wananchi wengi walitaka kupiga Kura mahali popote walipo. Kuwepo Sheria hii ni kuhakikisha kuwa kila mpiga Kura anajiandikisha katika Daftari mara moja na anapiga Kura mara moja katika kituo husika.
Kupiga kura katika kituo alichojiandikisha inawezesha kufahamu idadi halisi ya wakazi waliojiandikisha na kupiga kura na kuweka uwazi zaidi na Demokrasia ya kweli na kufanya uchaguzi kuwa wa kuaminika.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa