Home » » Tuna kila sababu ya kulinda na kuendeleza utamaduni wetu

Tuna kila sababu ya kulinda na kuendeleza utamaduni wetu




Benjamin Sawe
Maelezo
Dar es Salaam

Watu wengi katika jamii yetu ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na baadhi ya viongozi, vijana na watoto hawana uelewa mzuri kuhusu dhana ya utamaduni. Neno “Utamaduni” lina uwanda mpana na linaelezwa kwa namna tofauti na watu mbalimbali. Wataalamu, wanazuoni na wanajamii mbalimbali wametoa maelezo na tafsiri mbalimbali za dhana ya utamaduni. Tafsiri hizi tofauti zinatokana na sababu za kijiografia, kihistoria, kimazingira, kijamii na kipindi au muhula husika.


‘Utamaduni’ ni shughuli au kazi zote afanyazo mwanadamu na namna anavyokabiliana na mazingira yanayomzunguka ili kukidhi mahitaji yake muhimu ya kumwezesha kuishi. Mahitaji hayo muhimu ni Chakula, Makazi na Mavazi. Katika kumwezesha kupata mafanikio aliyotarajia katika kupata mahitaji hayo, binadamu alijiwekea utaratibu (nguzo) za msingi katika kutekeleza shughuli zake za kila siku.

Utaratibu (nguzo) huo ulikuwa ni ule wa kuandaa mazingira ambayo kila mtu alipaswa  kuyafuata kila mara anapofanya shughuli zake. Utaratibu huo ni ule wa kuwa na mila na desturi. Mila na desturi hizi ambazo mababu zetu wamekuwa wakizifuata kwa miaka mingi ni uridhi ambao tunapaswa kuuheshimu, kuulinda na kuuendeleza. Kwa maneno mengine, mila na desturi hizo ambazo ni sehemu ya utamaduni ni rasilimali muhimu sana katika maendeleo ya taifa letu.

Wahenga walinena ‘mkataa kwao mtumwa.’ Usemi huu unatufundisha mambo mengi sana ukizingatia mwenendo wa maisha ya Watanzania katika mazingira ya sasa. Kifupi, usemi huu una maana kwamba, mtu ambaye anadharau maisha na tamaduni ambazo amekulia nazo, ametekwa kimawazo na yuko tayari kutumikishwa au kufuata mila na desturi za jamii nyingine kutokana tu na tofauti ya tamaduni hizo.

Hivi sasa nchi yetu inasura mbili. Kuna sura ambayo inaonyesha jinsi ambavyo baadhi ya Watanzania baada ya kupata elimu yao, hususan elimu ya juu ambayo wameipata hapa nchini au nje ya nchi, wanajiona ni tofauti kabisa na Watanzania wengine. Wasomi hawa wanajiona wako katika nchi ngeni kabisa na sio ile waliyozaliwa.

Kundi hili linaonekana kudharau mila na desturi zetu na kuziona kama zimepitwa na wakati. Kundi hili ambalo linaonekana kuongezeka hapa nchini, linaonekana kutotambua na kutothamini kabisa utamaduni wetu na mchango wake kwa taifa. Mara nyingi kundi hili linaonekana likitumia lugha ya kigeni (Kiingereza) zaidi kuliko Kiswahili, kudhihirisha kuwa ni tofauti na jamii iliyopo.

Kuongea lugha ya Kiswahili kwao hujiona kama vile hawajaenda shule kabisa. Matokeo haya yanatokana na mwingiliano wa jamii zetu, kukua na kupanuka kwa nyanja ya mawasiliano na utandawazi. Aidha, kundi hili linatofautiana kabisa na jamii iliyopo kimavazi, aina ya chakula wanachokula na aina ya starehe wanazotaka.

Sura ya pili ya nchi yetu ni ile inayotambua kwamba utamaduni wetu ni muhimu sana katika kuifanya jamii ya kitanzania kuendelea kufuata mila na desturi katika shughuli mbalimbali za kulijenga taifa letu.

Jamii hii inalelewa na wazazi ambao bado wanaamini kuwa utamaduni wetu ni muhimu sana katika kuleta mafanikio mbalimbali ndani ya jamii. Mfano, nidhamu na kufuata mila na desturi zilizopo ambazo mababu na bibi zetu wamekuwa wakizifuata na kuweza kuiendeleza amani na utulivu katika jamii.

Historia ya nchi yetu inaonyesha kwamba, tangu tupate uhuru, kumekuwepo na amani na utulivu mkubwa katika jamii zetu. Sababu mojawapo ya msingi ni mshikamano uliokuwepo. Hata hivyo, msingi mkubwa wa kuwepo na mshikmano huo kulitokana na mawasiliano ambayo yalikuwa yakifanyika kwa kutumia lugha moja ya Kiswahili.

Licha ya kuwepo na lugha nyingine za makabila zaidi ya 120, wananchi walikuwa wakitumia zaidi lugha ya Kiswahili kwa mawasiliano katika shughuli mbalimbali. Kwa maana nyingine, lugha ya Kiswahili imeweza kuwaunganisha Watanzania wote na kuwa kitu kimoja na hivyo kuwa rahisi zaidi katika kufuata na kuuendeleza utamaduni katika jamii.

Kama nilivyosema hapo awali kwamba, Utamaduni ni muunganiko wa mila, imani na desturi ambazo kila jamii hufuata katika mwenendo wa maisha ya kila siku. Ili kuendeleza utamaduni wetu tunapaswa kuhakikisha kwamba, masuala ya matumizi ya lugha, mavazi, sanaa na burudani nk. Ni budi viende sambamba na utamaduni wetu.

Itapendeza zaidi kwa mtu mwenye uzalendo kuendelea kuheshimu mila na desturi ambazo zinajumuisha matumizi ya lugha, mavazi, vyakula vya asili, ngoma nk. Mambo haya ndiyo yatamfanya aweze kuwa tofauti na jamii ya nchi nyingine.

Hata hivyo, pamoja na ukweli kwamba baadhi ya mila na desturi hizo zimepitwa na wakati, zimesaidia sana kuilea jamii katika misingi ya utamaduni wetu na kuwa na nidhamu ya hali ya juu. Jambo la msingi hivi sasa ni kuhakikisha kwamba elimu zaidi inatolewa juu ya athari inayotokana na baadhi ya mila na desturi hizo potofu na kuendeleza zile ambazo bado ni msingi imara katika kuendeleza utamaduni wetu na kulijenga taifa katika misingi ya amani na utulivu.

Ni wazi kwamba, maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano na kuongezeka kwa utandawazi kumechochea zaidi mabadiliko yaliyopo katika jamii yetu katika nyanja ya utamaduni. Tofauti zilizopo katika suala zima la kufuata mila na desturi zinatokana na vijana wengi kujifunza kutoka nchi za kigeni.

Matumizi ya lugha ya Kiingereza hata pale ambapo kuna ujumbe muhimu kupitia sanaa mbalimbali kama vile muziki, maigizo, tamthilia nk.  inakuwa haina maana yeyote kwa jamii yetu kwa vile haitambui lugha hiyo. Wakati mwingine ujumbe kama huo umekuwa ukiposha jamii yetu. Aidha, Matumizi ya mavazi yasiyo na heshima yamechangia mambo mbalimbali kwa mfano, kuhamasisha vitendo viovu na vya kihuni kama vile ukahaba ubakaji nk.

Matumizi ya vyakula vya asili yana faida mbalimbali kwa binadamu katika kujingika na maradhi mbalimbali, kujenga na kuimarisha virutubisho vya mwili. Matumizi ya vyakula vilivyokaa kwenye majokofu kwa kipindi karibu wiki mmoja au zaidi vinapoteza radha yake ya asili na pia hata virutubisho vyenyewe vinapungua au kupoteza kabisa nguvu yake. Aidha vipo vyakula vilivyozalishwa katika mazingira yasiyo ya asili mfano kuku wa kisasa vimekuwa vyanzo vikubwa vya matatizo ya kiafya miongoni mwa watu.

Ukifanya uchunguzi wa haraka haraka utagundua kuwa, wazee wengi ambao wameishi kwa miaka mingi wamekuwa wakitumia zaidi vyakula vya asili ambavyo vimewasaidia sana katika kuiweka miili yao katika afya imara. Aidha amani na ututulivu katika jamii imechangia pia katika kutoa nafasi na uhuru mkubwa wa kufanya mambo mengi ya kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kilimo, ufugaji, uvuvi, na shughuli mbalimbali za kiutamaduni.

Wakati umefika kwa jamii zetu kutambua, kuenzi na kuendeleza tamaduni zetu ambazo tumezirithi kutoka kwa mababu na bibi zetu ili kizazi kipya nacho kiweze kufaidika na tamaduni hizo.


 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa