WILAYA ya Maswa, mkoani Simiyu imetekeleza agizo la Rais John
Magufuli la utengenezaji wa madawati kwa asilimia 75, asilimia 25
iliyobaki wameeleza kuikamilisha kabla ya Juni 30 mwaka huu.
Hayo yalisemwa jana mjini hapa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Rosemary
Kirigini wakati akisoma taarifa ya wilaya ya hali ya madawati katika
shule za msingi na sekondari kwa Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka.
Alisema wilaya hiyo inahitaji madawati 26,261 na hadi sasa madawati
yaliyopo ni 19,655, hivyo kuna upungufu wa madawati 6,606 na kwa shule
za sekondari mahitaji ya meza na viti yalikuwa ni 9,359 na yaliopo ni
10,810 na hivyo kuwa na ziada.
Kirigini alisema pamoja na mafanikio hayo wamekuwa wakikumbana na
changamoto mbalimbali zikiwemo za kukatikakatika kwa umeme, kasi ndogo
ya upatikanaji wa mbao, uhaba wa fedha na ushiriki mdogo wa wadau
mbalimbali katika kuchangia utengenezaji wa madawati.
Aidha alisema katika kutekeleza agizo hilo wilaya hiyo imejiwekea
mikakati ili kuondoa tatizo la upungufu wa madawati ambayo ni pamoja na
kukarabati madawati yote mabovu, kununua mbao 29,748 na kuzipeleka Chuo
cha Ufundi (Veta) cha Binza kilichoko wilayani humo.
Alisema Sh 475,968,000 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani ya halmashauri zitatumika kutengeneza madawati hayo.
Naye Mkuu wa Mkoa pamoja na kuwapongeza kwa ubunifu wa kukitumia Chuo
cha Ufundi cha Binza kutengeneza madawati, alisema huenda wilaya hiyo
ikawa ni miongoni mwa wilaya zitakazoongoza kwa utekelezaji wa agizo
hilo la rais.
Chanzo Gazeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment