Home » » Mashine zapunguza wasahihishaji 2,700

Mashine zapunguza wasahihishaji 2,700

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Imeandikwa na Maulid Ahmed, Dodoma.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya.
SERIKALI imesema tangu Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) lianze utaratibu wa kusahihisha mitihani kwa mashine, umepunguza wasahihishaji kutoka 3,000 hadi 300. Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya alibainisha hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) aliyetaka kufahamu lini serikali itapeleka bungeni marekebisho ya Sheria ya Necta ili Bunge kubadili Sheria ya Baraza Kifungu cha 20.
Katika kifungu hicho anataka kuondoa nguvu ya waziri wa Elimu ya kutoa maelekezo bila kuhoji na kushirikisha wataalamu wa elimu, kama kubadili aina ya mitihani hasa kuweka maswali ya kuchagua katika soko la Hisabati.
Alisema utaratibu wa kuchagua kwenye maswali ya Hisabati, umetokana na sasa utaratibu wa usahihishaji maswali ya mitihani kufanywa na mashine. Hata hivyo, wanafunzi wanapewa karatasi ya kufanyia mahesabu kupata majawabu.
Kifungu hicho cha 20 cha Sheria ya Baraza la Mitihani la Taifa, kinampa mamlaka waziri wa elimu kufanya maamuzi kwa niaba ya serikali, pale inapolazimika kufanya hivyo kwa kuzingatia mahitaji ya jamii kulingana na wakati, mazingira halisi na matokeo ya tafiti mbalimbali kutoka kwa wataalamu pamoja na maoni ya wadau wa elimu.
“Kwa kuzingatia matakwa ya Sheria hii, Baraza la Mitihani Tanzania hutakiwa kuyatekeleza maamuzi hayo,” alisema Naibu Waziri Manyanya. Manyanya alisema kwa sasa serikali haina mpango wa kufanyia marekebisho Kifungu cha 20 cha sheria hiyo kwa kuwa kinamwezesha waziri kufanya marekebisho mbalimbali kutokana na mahitaji ya jamii yanayojitokeza kwa wakati husika.
“Waziri hafanyi maamuzi kwa kukurupuka na si kila maamuzi yanatangazwa mengine hamuyasikii,” alisema. Mbunge wa Segerea, Bonnah Kaluwa (CCM) katika swali lake la nyongeza alitaka kufahamu lini serikali itatoa matokeo iliyoyazuia ya wahitimu wa kidato cha nne walioshindwa kulipa ada, kwani kwa sasa serikali inatoa elimu bure.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alimjibu “Tumelipokea na tutalifanyia kazi na majibu tutayaleta.”
Chanzo Gazeti la Habari Leo
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa