Home » » WADAU WA HABARI WAIPONGEZA SERIKALI.

WADAU WA HABARI WAIPONGEZA SERIKALI.


Na Abushehe Nondo, MAELEZO.
Wadau wa habari nchini wameipongeza Serikali kwa kuwasilisha   Bungeni Muswada wa Sheria ya Huduma za habari wa mwaka 2016.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri Tanzania (TEF) Bw. Theophil Makunga wakati akitoa  taarifa kuhusu muswada wa Sheria ya huduma za habari wa mwaka 2016 kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuanza mchakato wa kuiondoa sheria ya habari ya mwaka 1976 kwa kupeleka bungeni muswada mpya wa Sheria  ya Huduma za Habari wa mwaka 2016” Alisema Makunga.
Alisema kuwa muswada huo ambao umesomwa bungeni kwa mara ya kwanza na Waziri wa habari ,Utamaduni , Sanaa na Michezo Nape Nnauye utamaliza  kilio cha siku nyingi cha waandishi na wadau wa habari kuhusu sheria ya mwaka 1976 ambayo ilionekana kuwabana katika utendaji wao wa kazi.
Ameongeza kuwa   katika muktadha huo, taasisi mbalimbali za kihabari na wadau wa habari wanatakiwa kushiriki katika kutoa maoni yao ili kazi ya uandishi wa habari isiwe na matatizo.
Makunga amesisitiza kuwa  muswada huo siyo mali ya wamiliki wa vyombo vya habari , wahariri, au vyumba vya habari vilivyopo Dar es Salaam pekee bali unagusa maslahi mapana ya sekta nzima ya  habari nchini.
Aidha, katika kukusanya maoni hayo ya  wadau wa habari wamewekewa mpango utakaowawezesha kukusanya maoni yao nchi nzima  kupitia klabu zao za  waandishi wa habari  zilizosambaa  nchi nzima.
Wadau wa habari nchini wataweza kusoma muswada huo na kufanya uchambuzi wa maudhui yake na  hatimaye kutoa maoni yatakayowezesha kupatikana kwa sheria bora.
Muswada wa Sheria ya huduma za habari wa mwaka 2016 kwa mara ya kwanza umesomwa  bungeni   na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye katika Mkutano wa Nne wa Bunge la 11 lililomalizika  Septemba 16  mwaka huu.
MWISHO.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa