Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Dar es Salaam.
CHAMA cha Viziwi Tanzania (CHAVITA)chaiomba
Serikali kuandaa mkakati wa kuwawezesha walimu wa lugha ya alama kupata
utaalamu wa kuweza kufundisha watoto viziwi kutumia lugha hiyo.
Mwenyekiti
wa chama hicho Bw. Nadrosy Mlawa aliyasema hayo alipokuwa akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu maadhimisho ya
wiki ya viziwi duniani ambapo kitaifa yanafanyika mkoani Tanga.
Bw. Mlawa alisema kuwa mbali na hali ya maendeleo ya viziwi kuimarika kutokana na kukua kwa mwamko katika jamii na Serikali kwa ujumla pamoja na ushiriki wa wadau mbalimbali katika harakati za watu wenye ulemavu ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokuwa na wataalamu wa kufundisha watoto viziwi nchini.
“Kwa
sasa hali ya maendeleo kwa viziwi inazidi kuimarika kutokana na kukua
kwa mwamko katika jamii na serikali kwa ujumla, ushiriki wa wadau
mbalimbali katika harakati za watu wenye ulemavu umesaidia kuimarisha
hali hii tofauti na miaka ya 1990” alisema Bw. Mlawa
Aidha,
aliendelea kufafanua kuwa jamii imekuwa ikiunga mkono juu ya matumizi
ya lugha ya alama na kupenda kujifunza lugha hiyo ya viziwi, pia
kumekuwa na baadhi ya taasisi ambazo zinajali mahitaji ya viziwi na
kuchukua hatua ya utekelezaji wa mahitaji hayo.
Mbali
na hayo, Mwenyekiti huyo alisema kuna changamoto nyingi wazipatazo
viziwi kutegemeana na hali halisi ya mazingira, umri na shughuli
wazifanyazo ikiwemo kutofundishwa kwa lugha ya alama katika ngazi zote
za upatikanaji wa elimu.
Vilevile
ukosefu wa huduma ya ukalimani kwenye maeneo na matukio nyeti
yanawafanya viziwi kufadhaika na kuonekana kuwa hawawezi, hawaelewi,
wagumu na kutowajibika licha ya baadhi yao kuwa na taaluma mbalimbali.
Bw.
Mlawa aliendela kwa kusema kuwa kutotambuliwa kirahisi na utamaduni wa
kiziwi anayetumia lugha ya alama na kubambikiwa majina yanayodhalilisha
utu ni miongoni mwa changamoto wanazokumbana nazo katika jamii.
Kwa
upande wake Mratibu kutoka Chama cha Walimu wenye Uziwi Tanzania
Francis Mbisso alisema kuwa pamoja na uwepo wa mikakati, sheria, kanuni
na programu zenye matamko chanya bado utekelezaji wake unasuasua kwa
baadhi ya maeneo nchini.
Alisema
kuwa shule za viziwi na vitengo vya viziwi zimekuwa zikikosa
ufundishaji wa watoto viziwi kwa kutumia lugha ya alama ikiwa na sababu
kubwa ya walimu kukosa utaalamu wa lugha hiyo na kutegemea kujifunza
kutoka kwa wanafunzi wao.
Mbali
na hayo alitoa wito kwa jamii kwa ujumla wakiwemo waandishi wa habari
kujifunza lugha ya alama ili kuweza kuwasaidia na kuwapasha habari
zinazohusu jamii na huduma nyingine.
Wiki ya viziwi duniani huadhimishwa kila mwaka mwezi
Septemba ikiwa na lengo la kuonyesha jamii uwezo wa viziwi na
kuelemisha jamii changamoto wazipatazo kutokana na hali ya ulemavu wao
na jisni ya kuzishughulikia.
mwisho
0 comments:
Post a Comment