Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu, wametaka
kuundwa Tume ya uchunguzi wa mapato yatokanayo na ushuru baada ya
kushangazwa na kiasi kidogo cha fedha zilizokusanywa katika minada
mikubwa na tegemezi kwa halmashauri hiyo.
Hatua hiyo ni baada ya kupokea na kujadili taarifa ya kamati ya fedha
ya kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2015/2016 ya Oktoba hadi
Desemba iliyokuwa ikionesha hali mbaya ya ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Taarifa hiyo ilionesha kuwepo kwa baadhi ya minada ambayo ni mikubwa
katika halmashauri hiyo na tegemeo yenye zaidi ya watu 7,000, ikikusanya
Sh 4,000 hadi 11,000 kama ushuru wa matandiko, ng’ombe na mazao
mchanganyiko kwa muda wa mwezi mmoja.
Madiwani hao walionekana kushangazwa na hali hiyo wakati wa kikao cha
baraza la halmashauri kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, na
walidai kwa nyakati tofauti kuwepo kwa vitendo vya rushwa katika
ukusanyaji huo.
Kwa mujibu wa madiwani hao, minada mikubwa ya Dutwa, Nkololo, Masewa
na Ngulyati ambayo ni tegemeo kubwa kwa halmashauri hiyo, inaonesha
imekuwa ikikusanywa Sh 4,000 hadi 11,000 mara nne katika kipindi cha
mwezi mmoja huku mingine ikiwa haina kiasi chochote cha fedha
kilichokusanywa.
Walisema haiwezekani minada hiyo na mingine, pamoja na magulio zaidi
ya 20, ikusanye kiasi kidogo kama hicho, huku wakieleza kuwa wamekuwa
wakishuhudia zaidi ya tani 300 za mazao mchanganyiko zikibebwa katika
magari.
“Hapa kuna baadhi ya watumishi ambao ni wahusika katika ukusanyaji wa
ushuru, kodi hizi zinaishia katika mifuko yao lazima uchunguzi ufanyike
haiwezekani katika mnada au gulio yakusanywe matandiko ya watu wawili,
magunia yatozwe mawili pekee,” alisema Benjamin Holela.
Diwani wa Girya, Lewa Safari alisema amekuwa akishuhudia katika
minada ya Dutwa na mingine zaidi ya tani 300 za mazao na ng’ombe 600
vikitolewa ndani ya mnada huo lakini anashangazwa kuona kiasi kidogo
kilichokusanywa.
Alisema kuwa baadhi ya minada na magulio imekuwa haina mawakala na
hivyo halmashauri kupitia idara ya fedha hulazimika kukusanya yenyewe,
ambapo alisema inashangaza gari kuwekwa mafuta na watu kulipwa posho
kufuata ushuru, lakini wanarejea na kati ya Sh 4,000 na 11,000.
Akizungumzia hali hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Abdallah
Malela, alisema baadhi ya minada na magulio imekuwa na migogoro mikubwa,
hali inayoisababishia halmashauri kutokukusanya ushuru kabisa na wakati
mwingine kukusanya kiasi kidogo.
Aidha alisema minada mingi na magulio vipo chini ya halmashauri
lakini havina mawakala kutokana na baadhi yao kuvunja mikataba kwa
kushindwa kufikia kiwango cha makubaliano ya ukusanyaji wa ushuru katika
mikataba yao.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment