Na Benedict John-MAELEZO
3.2.2016
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simiyu Trasias Kagenzi amekanusha
madai yaliyoandikwa na baadhi ya vyombo vya Habari kuhusiana na taarifa
za kufanyika kwa mgomo unaotarajiwa kufanywa na baadhi ya Madaktari na
Wauguzi katika Hospitali mkoani Simiyu na kusema habari hizo sio za
kweli.
Kauli hiyo ameitoa
leo katika mahoajiano na Mwandishi wa Habari hii juu ya kuwepo kwa
mgomo huo ambapo alifafanua kuwa, taarifa hiyo haina ukweli wowote
kwani siku ya tarehe 02 Februari mwaka huu, alikuwa na kikao na
watumishi wote wa Hospitali hiyo ambapo kati ya mambo walioyajadili ni
stahili na hali ya kazi hospitalini hapo.
''Hapa wilayani
kwetu kuna baadhi ya waandishi ambao hawazingatii maadili ya kazi zao
hasa kwa kuandika habari zisizo na ukweli, nimeshangaa kusikia taarifa
hii kwasababu ukweli ni kwamba mimi nilikaa na watumishi wote jana
wakiwemo madaktari, wauguzi na madereva na moja ya mambo tuliyojadili ni
pamoja na mishahara yao na posho zao, na tulimaliza kikao chetu kwa
amani kabisa, sasa waandishi kama hawa tunawaita makanjanja maana haina
ukweli wowote'', alisema Kagenzi.
Aliongeza kuwa,
kitendo walichokifanya baadhi ya waandishi hao kuandika habari hiyo sio
jambo la busara kwani linaleta mkanganyiko na chuki baina ya watumishi
na viongozi wao na hata kwa serikali yao na amelaani jinsi waandishi hao
wanavyotumia kalamu zao vibaya kwa kupotosha umma wa watanzania.
''Inasikitisha kwa
kweli mtu anakurupuka bila kuwasiliana na Utendaji Mkuu wa Hospitali na
kuanza kuanza kukutana na madaktari anaowajua na kuanza kuandika
taarifa kama hizi na kuzirusha katika vyombo vya habari'', alisisitiza
Kagenzi.
Mkurugenzi huyo
amewataka waandishi wa habari kuzingatia maadili ya kazi zao ili waweze
kuandika habari ambazo zinatoa picha halisi badala ya kuwaogopesha
wananchi na hivyo kushindwa kwenda kupata huduma.
Kwa upande wake
Afisa Habari wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Bi. Stella Kalinga alieleza
kuwa baada ya kufuatailia taarifa aligundua kuwa siyo za kweli kwani
hakuna dalili yoyote ya mgomo kwa watumishi hao wa afya na wako kazini
wakiendelea na majukumu yao kama kawaida.
0 comments:
Post a Comment