MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji mstaafu Francis Mutungi, amevitaka vyama vya siasa nchini na watangaza nia wa nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu, kujiepusha na vitendo vya kuwarubuni au kuwanunua wapigakura.
Pia aliwataka wagombea wote, kuisoma Sheria ya Gharama za Uchaguzi ili kuzingatia matakwa yake na wakikiuka, wanaweza kupoteza sifa za kuwania uongozi wanaoutaka.
Jaji Mutungi aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari akisema Sheria ya Gharama za Uchaguzi, imetoa mwongozo wa fedha ambazo wagombea watazitumia kwenye kampeni zao.
Alisema lengo la sheria hiyo ni kudhibiti matumizi ya gharama za uchaguzi ambapo sheria hiyo inampa msajili jukumu la usimamizi na utawala wa gharama za uchaguzi.
"Sheria hii inasema wazi kuwa, chama cha siasa kitagharimu mchakato wa kura ya maoni na kampeni za uchaguzi, hii ni pamoja
na gharama zote ambazo zitatumika kwa ajili ya uhamasishaji ili kumnadi mgombea kwa wapigakura, gharama za chakula, vinywaji, malazi na usafiri," alisema Jaji Mutungi.
Aliongeza kuwa, wagombea ambao watabainika kujihusisha na vitendo vinavyoonekana kuleta hisia za kununua au kurubuni wapigakura, watakuwa wamekiuka utaratibu.
Alisema kama chama chake kitapuuza ukiukwaji huo na kumpitisha mgombea kuwania uongozi, sheria hiyo inampa mamlaka Msajili kumwekea pingamizi.
"Pia sheria hii imeweka viwango vya gharama za uchaguzi vikizingatia tofauti ya majimbo, idadi ya watu na miundombinu
ya eneo husika na kwa mgombea urais ambaye hatakiwi kutumia zaidi ya sh. bilioni mbili," alisema.
Vikundi vya ulinzi
Hata hivyo, Jaji Mutungi alivitaka vyama vya siasa ambavyo vinamiliki vikundi vya ulinzi ambavyo vinapatiwa mafunzo ya kijeshi, kuvivunja mara moja kwani ni kinyume na sheria za nchi.
Alisema kisheria, Katiba na kanuni za vyama vya siasa hazipaswi kupingana na sheria za nchi; hivyo kama katiba na kanuni zao zina
ibara inayopingana na sheria za nchi, ibara na kanuni hiyo ni batili.
Jaji Mutungi alisema vikundi vilivyopo kwenye vyama vya siasa kwa sasa ni tofauti na matarajio yaliyokuwepo awali mwaka 1992 kwa kupewa mfumo wa kijeshi, ukakamavu na kupeana vyeo vya kijeshi jambo ambalo ni ukiukwaji wa sheria za nchi.
0 comments:
Post a Comment