Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Uzoefu wangu wa kufuatilia masuala ya elimu, unaonyesha aghlabu matatizo mengi katika sekta ya elimu yanasababishwa na Serikali kama mdau mkuu.
Matatizo hayo yanatokana na na ama sera na mipango mibovu, au kutokuwepo kwa utekelezaji madhubuti wa mipango bora iliyobuniwa kuendeleza sekta hiyo muhimu kwa Taifa.
Huu ndio ukweli na kwa kiasi kikubwa Serikali kama msimamizi mkuu wa elimu, haiwezi kujitenga na lawama kuhusu matatizo yanayotokea katika sekta ya elimu.
Hata nyumbani watoto wanapokuwa watovu wa adabu, wa mwanzo kunyooshewa vidole ni wazazi ama walezi wao.
Ukweli ni kuwa elimu yetu imeshindwa kutengemaa kwa muda mrefu. Kuna viashiria mbalimbali vinavyoonyesha kuwa elimu inayumba, imejaa migogoro inayohatarisha mustakbali wa sekta hii mama nchini. Matokeo mabaya ya mitihani ya Taifa ni mojawapo ya viashiria hivyo.
Wajibu wa wananchi
Hata hivyo, wakati Serikali ikitupiwa mzigo mkubwa wa lawama kwa kushindwa kuisimamia ipasavyo sekta ya elimu, swali la kujiuliza ni; kwa kiasi gani wananchi tunafanya jitihada binafsi au za pamoja kuisaidia Serikali kuiendeleza elimu yetu?
Tuachane na masuala ya sera, mipango na mikakati ya kiserikali iliyo nje ya uwezo wa wananchi. Hebu kwa mfano, tujiulize mimi na wewe tunafanya nini kuhakikisha shule wanazosoma watoto wetu zinafanya vizuri kitaaluma.
Je, mazingira katika shule zetu yanakidhi haja ya kuwa mazingira sahihi kwa utoaji wa elimu? Tunawasimia vipi walimu kuwajibika na hata kuwahimiza watoto wetu kujifunza kwa bidii shuleni na nyumbani?
Ieleweke shule ninazokusudia hapa ni zile za umma, zenye idadi kubwa ya watoto wa nchi hii. Hivi sasa usimamizi wa shule hizi umegatuliwa, wamepewa wananchi kupitia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Katika maeneo mengi nchini, kuna ushiriki mdogo wa wazazi katika maendeleo ya shule wanazosoma watoto wao. Kibaya zaidi ni pale wazazi wanaposhindwa hata kufuatilia maendeleo binafsi ya watoto wao.
Si ajabu kukuta shule yenye wanafunzi zaidi ya 600, wazazi wanaohudhuria mikutano ya shule hawazidi 100. Mikutano hii ndiyo majukwaa ya kujadili masuala mbalimbali, lakini wazazi na walezi wanaisusa.
Tutaendelezaje elimu na kusimamia uwajibikaji shuleni kama wazazi ambao ni wadau muhimu hatuhudhurii vikao?
Tutayajuaje matatizo ya shule na watoto wetu na namna ya kuyatafutia ufumbuzi, kama kila siku tunawatuma watumishi wa ndani au vijana wa mtaani watuwakilishe kwenye vikao, kisa tumetingwa na shughuli za kimaisha?
Ushahidi wa tafiti
Hata tafiti zinaonyesha kuwa ushiriki wa wazazi katika masuala yanayohusu shule wanazosoma watoto wao hauridhishi.
Moja ya tafiti hizo ni uchunguzi wa mwaka 2010 kuhusu utoaji wa huduma za jamii uliofanywa na Uwezo iliyo chini ya asasi ya Twaweza.
Ripoti ya utafiti huo uliotumia sampuli ya baadhi ya wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam, inasema wazazi wengi hawajui sera, mipango ya kielimu na hawana uelewa wa mambo mengi kuhusu elimu ya watoto wao shuleni.
“ Karibu nusu tu ya wazazi ndio waliosema wanafuatilia maendeleo ya elimu ya watoto wao katika baadhi ya mambo kama kuhudhuria mikutano ya kamati za shule na kuzungumza na walimu kuhusu maendeleo ya watoto,’’inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Kwa hali hii, tukubali kuwa nasi wazazi na wananchi kwa jumla tunachangia kurudisha nyuma maendeleo ya elimu nchini.
Mtoto anasoma shule ya msingi kwa miaka saba, mzazi hujawahi kwenda shule hata mara moja kuzungumza na walimu kuhusu maendeleo yake. Matokeo yakiwa mabaya, mzazi huyuhuyu ndiye anayechochea mjadala baa au au katika vijiwe vya kupiga soga kuwa Serikali haiwajibiki.
Ukweli unabaki kuwa wazazi na walezi wengi hatutimizi wajibu wetu iwe kwa shule au kwa watoto wetu. Tunasubiri mambo yaharibike na kuanza kuwatupia lawama walimu au kuinyooshea kidole Serikali kama vile ndiyo chanzo pekee cha matatizo ya elimu yetu.
Natambua kuna mahala Serikali inapatia na pia inapokosea, lakini mimi na wewe tunaisaidiaje ili isiendelee kukosea? Tuwajibike kwa maendeleo ya watoto, kwani hao ni wetu na sio wa Serikali.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment