Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba.
Wakati
bado haijafahamika lini mgombea urais kupitia vyama vinavyounda Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) atatangazwa rasmi, imefahamika kuwa
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba, amekuwa
ndiyo kikwazo cha kutopatikana kwa mgombea huyo.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE kwa siku nne sasa umebaini kuwa
hatua ya Profesa Lipumba kukwepa vikao vya Ukawa, ni mkakati mahsusi
unaolenga kukwamisha mchakato wa kupatikana mgombea urais wa umoja huo.
Ukawa unaundwa na Cuf, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi na NLD.
Taarifa kutoka ndani ya vikao vya Ukawa vimeeleza kuwa kikao cha
kwanza cha umoja huo, Profesa Lipumba aliulizwa kwanini anataka kugombea
urais na kujibu kuwa anaamini kuwa yeye ndiye bora kuliko wengine.
Hata hivyo, alipoulizwa kama amejiandaa vipi kirasilimali iwapo
atateuliwa kuwania nafasi hiyo kupitia Ukawa, hakuwa na majibu ya
kujitosheleza na badala yake ilibainika kuwa Cuf imejiandaa zaidi
Zanzibar kuliko Tanzania Bara.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Profesa Lipumba amekuwa aking’ang’ania
agombee urais na hata mkutano wa mwisho wa Ukawa ambao hakuhudhuria,
inadaiwa kwamba ni mkakati wa kushinikiza ateuliwe yeye kugombea nafasi
hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.
Tangu Alhamis wiki iliyopita, gazeti hili limekuwa likimtafuta
Profesa Lipumba atoe ufafanuzi wa madai yanayotolewa kwamba anakwamisha
mchakato wa kumpata mgombea urais, lakini simu yake imekuwa ikiita bila
kupokelewa na hata akitumiwa ujumbe mfupi wa maneno, hajibu.
Ofisa Habari wa Cuf, Silasi Mpinga, alipoulizwa namna gani Profesa
Lipumba atapatikana kujibu madai hayo, alisema aendelee kutafutwa tu
atapatikana.
Katika vikao vya Ukawa, hoja kubwa imekuwa ni suala la mgombea
urais, nafasi ambayo inawaniwa na Profesa Lipumba ambaye tayari
ameshachukua fomu kupitia chama chake cha Cuf pamoja na Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk. Willibrod Slaa, anayeungwa mkono na vyama vyote vinne.
Profesa Lipumba ameshagombea urais mara nne bila mafanikio, wakati
Dk. Slaa aligombea mwaka 2010 na kushika nafasi ya pili, akiwa
ameitikisa CCM iliyopoteza asilimia takriban 20 ya kura za mwaka 2005.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia, akizungumza na waandishi
wa habari Julai 14, mwaka huu, alisema umoja huo utamtangaza mgombea wao
wa urais baada ya siku saba ambazo zinaisha wiki hii.
Alisema wamekubaliana kutangaza mgombea baada ya siku saba ili
kutoa nafasi kwa viongozi walioshiriki majadaliano hayo kutoa taarifa
kwa wanachama wa vyama vyao juu ya mambo waliokubaliana.
Aidha, Mbatia alikanusha uvumi kuwa kada wa CCM na Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa, ana mpango wa kujiunga na umoja huo ili apewe
nafasi ya kugombea urais baada ya kukosa nafasi hiyo kupitia chama
chake.
Mbatia pia alikanusha uvumi ulioenea kwenye mitandao ya kijamii
kuwa kuna mvutano mkubwa ndani ya Ukawa katika suala la mgombea urais
ambao umesababisha Cuf kutaka kujitoa.
“Hakuna ukweli katika hilo na hata leo (jana), nimeongea na Profesa
Lipumba kumtaarifu hatua tulioyofikia, hivyo hakuna mpasuko wowote,”
alisema Mbatia.
Kabla ya taarifa hiyo ya Mbatia,Ijumaa iliyopita Ukawa walitoa
taarifa ya kwamba wangemtangaza mgombea wake ndani ya saa 24, ahadi
ambayo haikutimizwa.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment