Home » » Vita ya urais yashika kasi mtandaoni

Vita ya urais yashika kasi mtandaoni


  Wakati safari ya kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu ikipamba moto, kumeibuka makundi ya watu yaliyofungia akaunti katika mitandao ya kijamii yakiwaunga mkono baadhi ya wanasiasa waliotangaza au wanaotajwa kuwa na nia ya kugombea urais ya kuwashambulia washindani wao.
Kila kundi limejipatia wafuasi wengi ambao wanaonyesha kumkubali mwanasiasa husika wanayedhani anafaa kuwa rais wa Tanzania endapo atapitishwa na chama chake na kupigiwa kura na wananchi.
Hata hivyo, wasomi na wachambuzi wanaonya kuwa pamoja na njia hii kuwa ya haraka kuwafikia wapigakura walio wengi ambao ni vijana na wanawake, inatakiwa kutumika kwa uangalifu la sivyo inaweza kusababisha machafuko.
Makundi yenyewe
Makundi hayo, mengi yakipatikana katika mitandao ya Facebook, Twitter na WhatsApp yanafanya kazi ya kuwanadi wanasiasa na kubainisha shughuli mbalimbali wanazozifanya kila siku wawapo katika ziara zao za binafsi, za kiserikali au kichama katika maeneo mbalimbali nchini.
Baadhi ya kurasa za makundi hayo zenye wafuasi wengi ni pamoja na ule wa ‘Team Lowassa’, kundi linalomuunga mkono Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambao hadi jana ulikuwa na wafuasi 46,124 ambao wanaweza kupata habari mbalimbali zinazomhusu kiongozi huyo.
Hata hivyo, mbunge huyo ambaye pia aliwahi kuwa waziri mkuu, hivi karibuni alikaririwa na gazeti hili akiikana moja ya akaunti za Twitter iliyokuwa imechapisha taarifa zilizomkariri akizungumzia suala la ufisadi wa escrow.
Akizungumzia kurasa hizo, Msaidizi wa Lowassa, Abubakar Liongo alisema akaunti hizo zinatengenezwa na marafiki na kusisitiza kwamba kiongozi huyo hahusiki nazo kwa namna yoyote.
“Hawa ni marafiki tu, huwezi kuwazuia kufanya wanachotaka kufanya, sisi tumeshatoa taarifa kuwa hizi hatuhusiki nazo,” alisema Liongo.
Kundi jingine linajitambulisha kama ‘Team Hamis Kigwangalla’ linalomuunga mkono Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla na mpaka kufikia jana lilikuwa na wafuasi 9,893. Hili ni kundi la pili kuwa na wafuasi wengi katika mtandao wa Facebook baada ya lile la Team Lowassa.
Ukurasa mwingine umeanzishwa na watu wanaomuunga mkono Mbunge wa Bumbuli na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba. Ukurasa huu umepewa jina ‘January Makamba – The next President’ na hadi jana ulikuwa na wafuasi 7,075.
Wanasiasa wengine wanaohusishwa na mitandao hiyo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye mbali na akaunti yake kwenye WhatsApp, ukurasa wa marafiki zake kwenye Facebook wenye jina la ‘Bernard Membe Fans Page’ umefikisha wafuasi 5,120.
Kundi la wafuasi wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa linafuatia. Kundi hilo lililoanzisha mtandao uliopewa jina ‘Dr Slaa Team Winner – 2013/2015’ hadi jana lilikuwa na wafuasi 4,337.
Vilevile, lipo kundi jingine linalomuunga mkono Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira na ambalo ukurasa wake uitwao ‘Wasira wa Watanzania (WWW)’ lina wafuasi 3,524.
Pia upo ukurasa wa “Marafiki wa Samwel Sitta’ katika Facebook wenye mashabiki 2,238 wanaomuunga mkono Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Katika mtandao wa Twitter, wanasiasa hao na wengine hawako nyuma, karibu kila mmoja ana akaunti binafsi huku wafuasi wao wakipata nafasi ya kusoma yale wanayoyaandika wakati wowote.
Miongoni mwa wanasiasa wenye wafuasi wengi ni Zitto Kabwe ambaye watu 208,294 wanafuatilia hoja zake na wakati mwingine kujibizana.
Anayefuata ni Makamba mwenye wafuasi 151,822, Bernard Membe (45,889) na Dk Slaa (40,830). Lazaro Nyalandu aliyetangaza wiki iliyopita kuingia katika mbio za kusaka urais, akaunti yake ya Twitter inafuatiliwa na watu 36,726.
Wengine katika mkondo huo ni Dk Khamis Kigwangalla (26,322), William Ngeleja (11,110), Anna Tibaijuka (8,053), Freeman Mbowe (4,162), Asha-rose Migiro (4,736), Edward Lowassa (2,123), Stephen Wasira (750) na Dk Emmanuel Nchimbi (515).
Ni dhahiri kuwa wanasiasa vijana ndiyo wanaotumia zaidi mitandao ya kijamii na kuwa na wafuasi wengi ambao wengi wao pia ni vijana.
Maoni ya wachambuzi
Baadhi ya wasomi nchini wameelezea kuwa si jambo baya kutumia mitandao ya kijamii kujinadi kwa wananchi. Hata hivyo, wameonyesha wasiwasi kwa jinsi inavyotumika na kuwa inaweza kusababisha machafuko.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Hamad Salim alisema kadri muda unavyokwenda, ndivyo jamii inavyobadilika na mabadiliko haya yanahusisha pia matumizi ya mitandao ya kijamii.
Salim alisema vijana na wanawake ambao ndiyo idadi kubwa ya wapiga kura, sasa wanatumia mitandao ya kijamii. Alisisitiza kuwa hii ndiyo sababu pekee iliyowasukuma wanasiasa kuanza kutumia mitandao ya kijamii.
“Mitandao hii inawasaidia wanasiasa kujitangaza kwa wananchi, pia haina gharama kwao. Tulizoea kuona wanasiasa wakipita mitaani kutoa zawadi na kujinadi kwa wananchi kipindi cha uchaguzi, sasa ni rahisi,” alisema.
Hata hivyo, Salim alionya kuwa mitandao ya kijamii isipodhibitiwa kikamilifu, inaweza kusababisha machafuko ya kisiasa kama ilivyotokea katika nchi za Tunisia na Libya na kusababisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yanaendelea mpaka sasa.
“Tuliona pia wakati wa sakata la escrow, watu walianza kuunda baraza la mawaziri mtandaoni kabla hata Rais hajasema chochote. Sasa hii ni hatari, wakati mwingine inaweza kujenga chuki,” alisema.
Alisema katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika hivi karibuni, Ukawa hawakutumia nguvu kubwa kwa sababu walishajenga ngome kwenye mitandao ya kijamii.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema sasa hivi mitandao ya kijamii ni sehemu ya maisha ya Watanzania. Hivyo, inakuwa rahisi kwa wanasiasa kuwafikia wengi ndani ya muda mfupi kwa njia hiyo.
Alisema uzuri wa mitandao ya kijamii ni kuwa wanasiasa wanapata nafasi ya kujitangaza na wananchi pia wanapata kuwafahamu na kuwapima kama wanaweza kuongoza Taifa hili.
Aliuangana na Salim akisema kuwa Tanzania haina udhibiti mzuri wa mitandao ya kijamii, jambo linaloweza kusababisha chuki na mifarakano miongoni mwa wanajamii.
“Si kila linaloanzishwa ni jema asilimia 100, wengine wanatumia mitandao ya kijamii kuwachafua wengine, hasa mahasimu wao kisiasa,” alisema Mbunda na kuitaka Serikali kuwa na udhibiti wa mitandao hiyo hasa wakati huu kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Vijimambo Blog
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa