Home » » MITANDAO YA KIJAMII NA CHANGAMOTO KWA USALAMA WA TAIFA LETU-3

MITANDAO YA KIJAMII NA CHANGAMOTO KWA USALAMA WA TAIFA LETU-3

Leo nahitimisha mfululizo wa makala haya. Licha ya mitandao ya kijamii kuweza kutumika dhidi ya usalama wa Taifa, pia inaweza kulinda usalama wake na wananchi tena kwa ufasaha zaidi.
Hata hivyo, hilo linategemea namna mitandao hiyo itakavyotumiwa na wafanyakazi katika idara za Serikali na vyombo vilivyopewa dhamana ya kuihakikisha nchi inakuwa na ulinzi na usalama.
Kimsingi, vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kuwa tayari wakati wote kujibu au kusema kinachotolewa dhidi yao ili kupunguza madhara yanayoweza kutokea hasa pale vyombo hivyo vinaposhambuliwa katika mitandao ya kijamii.
Hili la vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua mapema tunaweza kuliona kwenye vurugu kati ya wakulima na wafugaji zilizowahi kutokea siku zilizopita na hata zinazoweza kutokea.
Tunakumbuka sote kuwa yalipotokea mauaji kati ya wakulima na wafugaji, baadhi ya watu walisambaza picha za mauaji hayo kwenye mitandao ya kijamii. Hili lilitokea huku Jeshi la Polisi likiwa limekaa kimya.
Pia vurugu za wilayani Siha na propaganda ya Wamasai kuhamishwa kutoka sehemu zao kwa ajili ya wawekezaji, taarifa zote hizi zilisambaa mapema kwa kutumia mitandao ya kijamii.
Ukweli ni kuwa kama vyombo vyetu vitaamua kufanya kazi kwa umakini na kwa weledi, vina uwezo mkubwa wa kudhibiti matumizi yasiyofaa ya mitandao.
Ilivyo ni kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinaweza kufanya utafiti na kukusanya taarifa nyingi zaidi kuhusu matukio yanayoweza kutokea na kuyakabili mapema zaidi kabla ya kuleta madhara kwa taifa.
Mathalan watumiaji wote wa mitandao ya kijamii huacha alama wanapotumia kama ni majina, picha au hata taarifa nyingine mbalimbali.
Taarifa hizi na nyinginezo zinaweza kukusanywa na kutumika na vyombo hivi kushugulikia mambo mbalimbali yanayoweza kuiathiri jamii. Hivi ndivyo tunavyoweza kuwagundua wahalifu au watu wanaotumia vibaya mitandao dhidi ya usalama wa Taifa na wananchi kwa jumla.
Katika nchi zilizoendelea idara za Serikali hasa majeshi na polisi yamewekeza kwenye mitandao ya kijamii kwa kutumia kampuni binafsi, ili ziwatengenezee programu mbalimbali zakufuatilia taarifa za matukio na watu kwa ajili ya matumizi ya majeshi na idara zao za usalama wa taifa .
Kama kweli tunataka kushindana na kuwa juu kwenye uwanja huu wa taarifa na maarifa kwa kutumia mitandao ya kijamii, nchi inatakiwa kuunda mfumo wa kitaasisi kwa ajili ya upatikanaji wa taarifa kwanza ndani ya idara zake zenyewe na pia nje ya idara
Nimewahi kuona jinsi jeshi la polisi linavyoshiriki kwenye makundi ya WhatsApp kwa polisi ili kupashana habari na matukio mbalimbali kwa njia ya picha, video na mambo mengine.
Utaratibu huu unasaidia kwa kiwango kikubwa kupashana taarifa za haraka hasa yanapotokea matukio ya ajali, wizi na hatari nyingine mbalimbali.
Kwa njia hii huhitaji redio ya upepo kusambaza taarifa kwa haraka miongoni mwa makundi au watu wanaolengwa.
Teknolojia ya mitandao inatosha kufanya kazi yake katika mazingira kama haya na walengwa wakafanyia kazi taarifa kwa haraka na kwa ufanisi wa hali ya juu
Chanzo:Mwananchi

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa