Profesa Anna Tibaijuka, aliyekuwa waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Tukiacha pembeni sakata hili la Escrow ambapo Profesa Anna Tibaijuka, ameondolewa kwenye uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , huku Profesa Sospeter Muhongo akiwa ameachwa kiporo na Rais Jakaya Kikwete. Swali la kujiuliza ni kweli kwamba maprofesa hapa nchini wameshindwa kuzimudu majukumu yao au kwasababu wamevamia taaluma isiyowahusu.
Nimelazimika kuweka jambo hili hadharani kwasababu hadhi ya “uprofesa” ni lulu kwenye anga za wasomi. Aidha, profesa kutoka Tanzania ana hadhi sawa na wengine kutoka barani Asia, Amerika, Uarabuni na Ulaya.
Ikumbukwe kwamba katika kipindi cha utawala wa hayati Mwalimu Julius Nyerere, maprofesa waliokuwepo walikuwa ni wachache. Sidhani kama waliweza kufika hata watano.
Ijapokuwa idadi ya maprofesa ilikuwa ikiongezeka kwa kasi, hata hivyo haikuwa jambo la kawaida kusikia wasomi hawa wakiimezea mate tasnia ya siasa. Inadhaniwa kuwa wasomi wa ngazi za shahada za uzamili hadi uprofesa walikuwa wakichukulia siasa kama vile imesheheni watu waongo, washereheshaji au wasanii.
Kwa msingi huo, ilikuwa ni vigumu kumpata msomi mwenye shahada ya uzamili ama uprofesa akihangaika kujiunga na siasa. Pengine kwa wale tu waliokuwa wamesomea taaaluma ya Sayansi ya Siasa.
Kashfa ya IPTL ni sawa na historia inayojirudia siyo mara ya kwanza kashfa ya aina hii kutokea hapa nchini, na mbaya zaidi imekuwa ikiwahusisha wasomi wa ngazi za juu hasa maprofesa.
Hii hapa chini ni orodha fupi ya maprofesa waliowahi kuingia kwenye tasnia ya siasa na kujikuta wakiambulia kuondolewa madarakani, marehemu Kigoma Malima, Simon Mbilinyi, Philimon Sarungi, Juma Kapuya , Peter Msolwa, David Mwakyusa, Tibaijuka na Muhongo amewekwa kiporo.
Wengine wanaosuasua ni Profesa Abdallah Safari na mwingine ni Ibrahim Lipumba huyo ameshindwa urais mara nne.
Tujiulize je kushindwa kwa maprofesa kutofanya vizuri katika tasnia hii ya siasa kunasababishwa na elimu yao kuwa kubwa zaidi kulinganishwa na majukumu ya kisiasa au kunasababishwa na ugumu wa kushindwa kwao kutafsiri elimu katika nadharia kwenda kwenye vitendo!
Tunapochambua sakata la akaunti ya Escrow, ni vizuri tukarudisha fikra zetu nyuma na kuelewa kuwa chimbuko la haya yote kadhia hii matokeo ya Sera ya Azimio la Zanzibar iliyolizika rasmi Azimio la Arusha lililokuwa na itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea na kuingiza siasa za kiliberali.
Ikumbukwe kuwa Azimio la Arusha katika kuanisha sifa nyingine za nchi lilisisitiza umuhimu wa kila mfanyakazi kupata “pato la haki kwa kazi aifanyayo na kwamba mapato ya wafanyakazi hayatofautiani mno”.
Maana ya dhana ya malipo halali ilielezwa kuwa ni kila mtu afanye kazi “kwa kadri ya uwezo wake na alipwe kulingana na mchango wake”.
Mwaka 1991, February Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ilikutana Zanzibar na kufanya mapitio ya katiba na baadhi ya sera za chama katika kile kilichoitwa “kujiandaa kuingia katika mfumo wa siasa ya vyama vingi”.
Sambamba na hilo, ingawa kikao hicho kilipitisha maamuzi mengi ya msingi lakini kikubwa kilichofikiwa ni “uamuzi wa kutenganisha sifa za uanachama na miiko au maadili ya viongozi wa chama”.
Huu ndiyo ukawa mwanzo wa kuwabariki wafanyabiashara kupata faida kubwa na wafanyakazi kupata malipo ya ziada.
Wadadavuzi wa mambo ya siasa wanasema, ufisadi wa Escrow ni ishara tosha kuwa sasa wafanyabiashara wameamua kutoa makucha yao wazi wazi.
Kwa maana nyingine ni kwamba nchi yetu sasa imeanza kuvuna kile ilichopanda baada ya kuingia rasmi kwenye mfumo wa kibepari.
Kama ilivyo ada, nchi zinazofuata mfumo wa siasa za kibepari hasa za Magharibi ikiongozwa na Marekani, wafanyabiashara ndiyo wanamiliki wa njia kuu za uchumi tofauti na mfumo wa kijamaa ambapo njia hizo zinamilikiwa kwa pamoja chini ya usimamizi wa dola.
Kwa tafsiri hiyo, wasomi wetu hao maprofesa baada ya kuona milango imefunguliwa rasmi na Azimio la Zanzibar mwaka 1991, wakaanza kutafuta malisho yanayolipa vizuri, hatimaye wakajikuta wakiingia kwenye tasnia ya saisa bila maandalizi ya kutosha.
Nasema bila ya maandalizi kwasababu duniani kote siyo jambo la kawaida kuwapata maprofesa wakiangaika kutafuta lishe nzuri kutokana na taaluma zao kujiuza popote.
Tofauti na hapa kwetu, maprofesa wengi walijikuta taaluma zao hazilipi hivyo, waliamua kujiingiza katika siasa kinadharia bila ya kujua undani wake kivitendo.
Matokeo yake wengi wao wamejikuta wakiambulia kashfa na kuondolewa kwenye viwanja vya siasa kwa aibu.
Ndiyo maana leo hauwezi kushangaa kumsikia Mbunge akimwambia profesa mchana kweupe kuwa ni “Mwongo”. Vile vile hauwezi kushangaa wananchi hata wale wa ngazi za chini kielimu wakimzomea profesa.
Aidha, ndiyo maana leo hii utamkuta Profesa akipiga magoti chini kwa wafanyabiashara ili apate fungu la kumwezesha kuingia “mjengoni” profesa yupo radhi hata kuutupilia mbali usomi wake kwa sharti la kuabudu benchi ya ufundi waganga wa kienyeji ili mradi apate ubunge.
Nchi isipoweka tahadhari ya kutambua mchango wa maprofesa wetu, bila shaka tutaendelea kushuhudia mlolongo wa maprofesa, wakiacha taaluma zao na kukimbilia tasnia hii ya siasa.
Rai yangu kwa serikali ni kwamba, wasomi wetu hawa watengenezewe mazingira bora ya kazi ili wasirudi huku saiti kwenye tasnia isiyowahusu.
Wapewe hadhi zao kama walivyo maprofesa wengine duniani. Maprofesa ni tunu ya taifa. Kuwatengeneza maprofesa kunachukua miaka mingi na ni gharama kubwa.
Ombi langu kwa wasomi hawa chonde chonde rudini kwenye taaluma zenu huku kwenye siasa “kunanuka” msiache mbachao kwa msaala upitao.
Makala yameandikwa na John M. Kibasso
Simu: 0713 - 399004/ 0767- 399004
Email: jmkibasso@gmail.com
CHANZO:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment