Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Ni wazi kuwa kila moja wetu anatamani kuburudika bila kujali ni aina gani ya burudani anayotaka.
Kuna aina nyingi na tofauti za burudani. Kuna muziki wa taarabu, Injili, dansi, wa kizazi kipya hata muziki wa kiasili.
Katika kundi la burudani pia kuna sanaa za
maonyesho, ngoma, vichekesho hata filamu. Hizo ni baadhi ya burudani na
kila mmoja ana uchaguzi au mapenzi yake kwa aina moja au zaidi.
Lengo langu leo ni kuzungumzia burudani lakini
nikilenga zaidi upande wa filamu. Hapa nawapongeza waigizaji kwa kazi
nzuri. Tasnia inakuwa kila kukicha na mabadiliko yanaonekana ingawa siyo
kwa asilimia kubwa.
Mabadiliko kwa nchi inayoendelea kukua kama
Tanzania yanakuja taratibu, hivyo hata katika nyanja hiyo kasi ya ukuaji
wake ni hiyo hiyo.
Hata hivyo, naweza kusema kuwa mabadiliko yapo na kwa anayefuatilia anaweza kuona baadhi ya waigizaji walivyobadilika.
Ingawa tunajivunia kukua kwa filamu, lakini katika
kazi hiyo sasa, badala ya kulipeleka mbele gurudumu hilo, tunafikiria
kulirudisha nyuma. Sababu kubwa ya kulirudisha nyuma gurudumu la filamu
ni aina ya uigizaji na jinsi tunavyojichanganya katika uhalisia. Filamu
nyingi zinaigizwa bila kuonyesha uhalisia wa kilichokusudiwa.
Haiwezekani mwanzo hadi mwisho wa filamu
azungumziwe mtoto bila kuonekana hata katika kipengele kimoja. Hilo
linatokea kwenye filamu, huku wazazi wakilitumia jina lake katika
mazungumzo yao, wala hawasemi kama amesafiri au la.
Filamu bora ni ile yenye uhalisia, mtu anaposema
yupo kijijini, aonekane kweli yupo huko. Ni ngumu kuamini unapomwona
mhusika amekuja kutafuta kazi kwa mara ya kwanza mjini, lakini ametinda
nyusi na kubandika kucha. Akili yangu inanituma kuwa, filamu haiigizwi
usiku mmoja. Ni kitu kinachoandaliwa kwa muda mrefu, hivyo kuna haja ya
kuwa na maandalizi ya uhalisia hata ikibidi kufuga ndevu ikiwa
zitahitajika.
Msichana anapoigiza kuwa ametoka kijijini,
asitinde nyusi au kuvaa wigi. Ajiandae na kuonyesha uhalisia wa maisha
ya kijijini. Ni muhimu kufanya maandalizi ya kitu kilichopo mbele yake
ili kuvaa uhalisia akiaminisha mashabiki .
Kuna wakati moja ya filamu za bongo ilizua gumzo
kwenye mitandao ya kijamii. Ilionyesha mtu aliyeigiza ujambazi, eti
anavua viatu ili aingie ndani ya nyumba kufanya ujambazi. Jambo hilo ni
ajabu kuruhusiwa na watayarishaji wa filamu ikizingatiwa mazingira
halisi pale unapofanyika ujambazi.
Kuruhusu hali hiyo iende na kuonekana kwa
mashabiki au wateja wa filamu ni kuwaibia. Hiyo yote inaonyesha wengi wa
wasanii wanavyoshindwa kuuvaa uhusika. Kwa bahati mbaya filamu hiyo
ilihaririwa na kuwa tayari kwa ajili ya kuwafikia watazamaji na wadau wa
kazi hizo. Lakini jambo la kujiuliza; je, kazi ya wahariri wa filamu ni
ipi kama wanapitisha vitu kama hivi?
Nawahurumia kwa kuwa mwisho mnaubeba udhaifu wenu wazi mbele ya
jamii mnayotaka kuifunza, kuiburudisha lakini pia ninyi kupata kipato
kwa mauzo ya kazi zenu. Kataeni aibu hii kwa pamoja kwa kuwa ili malengo
yenu yatimie ni lazima tasnia hii iwepo na iwe na heshima. Lakini kama
mtashindwa kuilinda, mjiandae kutafuta kazi nyingine kwani hii itakuwa
imekwisha.
Hakuna atakayekubali kutupa fedha kila siku
kuangalia filamu zisizo na uhalisia. Haina ubishi kuwa, kinachoonekana
kwa wakati huo ni filamu iliyoigizwa sawa, lakini kutokana na mabadiliko
yaliyopo kwenye nyanja hiyo ni lazima kuwapo na uhalisia. Kuigiza
filamu bila kuwa na uhalisia ni kujiweka nyuma kwani upinzani uliopo
sasa katika nyanja hiyo ni mkubwa kutokana na dunia kuwa kijiji.
Tunakokwenda katika tasnia ya filamu, mwanga wa
mafanikio upo. Ni wakati wenu kuwa makini kabla hamjaleta aibu sebuleni
kwa wadau wenu.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment