Home » » WATUMISHI 6 WAPOTEZA KAZI MEATU KUTOKANA NA UTORO

WATUMISHI 6 WAPOTEZA KAZI MEATU KUTOKANA NA UTORO

                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                         
Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri
Watendaji watano wa vijiji na mmoja wa kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, wametimuliwa kazi kutokana na utoro pamoja na kudharau maagizo ya viongozi wa ngazi za juu wa wilaya hiyo.
Hayo yalibainishwa katika kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo mbele ya Mwenyekiti wa baraza hilo, Pius Machungwa.

Machungwa alisema watendaji hao wamefukuzwa kupitia Baraza la Madiwani wamekuwa wakituhumiwa kutokuwapo kazini kwa kipindi kirefu na jamii kushindwa kupata huduma yao.

Aliwataja watendaji waliofukuzwa kazi kuwa ni Shiwa Charles, wa kata ya Bukumbi, Paul Lalida, wa kijiji cha Nata, John Joseph, kijiji cha Baluli, Richard Matanga, wa kijiji cha Witamhinya na Charles Makaranga, Mtendaji wa kijiji cha Mwaga.

Aidha, madiwani wa halmashauri hiyo wamempa onyo kali Ofisa Ugavi Msaidizi, Emmanuel Marwa, kwa kosa la kudharau viongozi wa ngazi za juu pamoja na watumishi wenzake.

"Watendaji wote hao ni watoro kazini na walishaandikiwa barua za onyo ili kujirekebisha, lakini walipuuza barua za waajiri wao na hivyo Baraza likaamua kuwafuta kazi," alisema.

Aidha, alisema katika vijiji walivyokuwa watendaji hao vilionekana miradi yote ya maendeleo ‘imekufa’ kutokana na kukosekana usimamizi.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo amewataka watendaji wa vijiji na kata kusimamia kesi za migogoro ya mipaka ya shule za msingi na sekondari ili kuhakikisha inamalizika kwa haraka.

Alisema shule nyingi wilayani hapa zimekuwa na migogoro na wananchi ambao wanakaa katika mazingira ya shule ambao kesi nyingine zimepelekwa katika Mahakama ya Ardhi wilayani Maswa na kuiomba serikali kutuma wataalam wake kupima upya maeneo hayo.
CHANZO: NIPASHE
                                  

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa