Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kama unaingia kwenye ndoa kwa sababu ya kumkera fulani, fahamu
kwamba hilo ni kosa na linasababisha wakati fulani watu kujuta kwanini
amekutana na fulani.
Ingawa watu wanaweza kusema kwa kadri wanavyoweza,
ukweli ni kwamba utulivu kwenye ndoa kwa asilimia kubwa huletwa na
mwanamke. Utulivu huzaa mapenzi na huruma baina ya wanandoa, kwa maana
nyingine, mwanamke ana nafasi kubwa ya kujenga au kubomoa ndoa, hii
haina maana yake ni kwamba mwanamume hana nafasi ya uharibifu, bali
nafasi ya mwanzo inachukuliwa na mwanamke bila ya upinzani.
Sababu kubwa ya wanandoa kuchokana, au kuzeeka kwa
ndoa kunasababishwa na mwanamke, pale ambapo atashindwa kutumia nafasi
yake na vipawa alivyopewa kuleta utulivu katika ndoa yao, na hapa
nitajaribu kujadili baadhi ya visababishi vinavyopelekea kuzeeka kwa
ndoa au kuchokana. Visababishi ambavyo huwa vinadharaulika na kuonekana
vitu vidogo vidogo hususan kwa wanawake wengi.
Wapo ambao wanaweza kukanusha hili, lakini
unapaswa kujiuliza inakuwaje kama kweli mwanaume anashiba, kwanini aende
kusaka wanawake wengine kwa ajili ya kufanya nao ngono. Huenda akawa na
sababu nyingine, hata hivyo kwa asilimia kubwa hiyo humaanisha kwamba
huenda ndani ya ndoa yake kuna shida, hasa ya kupata kile ambacho
anakwenda kukitafuta nje.
Kuna wanawake wengi wamekuwa wakiwanyanyasa
wanaume kwa kauli zisizo nzuri…kama jana nilikupa na leo unataka kwani
mimi sichoki…nk. Ingawa inaonekana kama ni suala lisilo na maana, lakini
zungumza na wanaume wengi ambao wametoka tayari nje ya ndoa, mojawapo
ya sababu ni kutokuwa na uhakika wa kushiba katika ndoa zao. Hawapati
raha ile ambayo wanandoa wanastahili kupewa.
Kuna wanandoa wamekuwa wanaishi isivyo sawa,
kwamba wanaishi bila kuelewana vizuri. Kuelewana baina ya wanandoa ni
suala la msingi sana. Matatizo mengi ndani ya nyumba yanaweza
kusababishwa na moja au baadhi ya tabia za baadhi ya wanandoa, kwamba
mwingine anakuwa hana ukaribu au anafanya mambo ambayo hayamfanyi mmoja
kati yao kutokuwa na amani moyoni.
Wanapoanza uhusiano mwanamke kwa mwanaume, hujali
sana kuvaa vizuri, usafi wa mwili wake, usafi wa nyumba na nidhamu ya
hali ya juu. Aidha huwa ni kawaida kwa mwanamke kumuuliza mwenzi wake
anapenda kipikwe chakula gani na kadhalika. Hata hivyo kadri siku
zinavyokwenda mbele, si wanawake wengi huona umuhimu wa kuwauliza wenza
wao chakula cha kupika.
Wengi hupika chakula bila kuzingatia vionjo vizuri
wala kuwa na ubunifu. Wengine wamekuwa hawana mapokezi mazuri kwa wenza
wao. Lini uliwahi kumpokea mwenzi wako kwa kumpokea kwa kumkumbatia?
Kila aliyeko kwenye ndoa anapaswa kujiuliza hili.
Kuweni na mazungumzo
Mazungumzo ni njia muhimu ya kujenga ndoa na
kuiimarisha , aidha ni njia ya mkato ya kuchokana na kuchukiana.
Mwanamke ambaye hajui wakati gani aseme nini na wakati gani asiseme,
hujikuta katika wakati mgumu ndani ya ndoa yake.
Kama una mwanamke wa namna hii ambaye kila
anapoongea na mume wake huanza mazungumzo yake na matatizo na lawama
humfanya mumewe awe na woga kila anaposikia sauti yake, na kuiona nyumba
chungu, kwa sababu hakuna binadamu anayependa kusikia matatizo tu
wakati wote.
Ukweli mwanamke wa aina hii huwa anamsubiri mumewe
kwa hamu kubwa, na anapofika tu na kabla hata ya kupata rizki, anaanza
kumsomea orodha ya matatizo; watoto wamerudishwa shule, karo haijalipwa,
shangazi yako amepiga simu mjomba kalazwa Hospitali na kadhalika na
kadhalika. Nyumba ya aina hii huzeeka haraka na wanandoa kuchokana
Udhaifu mkubwa
Ni udhaifu mkubwa kwa wanandoa, kwamba baadhi yao
wamekuwa hawasomani na kujuana tabia. Bahati mbaya zaidi kuna wanandoa
ambao wamekuwa wakitaka tabia zao ndizo ziwe za kufuatwa katika ndoa
hata kama siyo nzuri. Kama unataka maisha mazuri ya ndoa, hakikisha
unaisoma tabia ya mwenzi wako na kujua na kwenda naye. Msingi wa kuwa na
maisha bora ya ndoa ni pamoja na kuifahamu kwa kina tabia ya mwenzi
wako na kuchukua hatua muafaka zenye lengo la kuimarisha uhusiano wenu.
Kwa mwanamke mwenye busara na mwenye kuithamini
ndoa yake, husoma tabia za mumewe na kuangalia jinsi gani anavyoweza
kuzioanisha na zile zake ili kuepusha migongano, aidha hutafuta fursa
muafaka ya kumkinaisha mumewe juu ya fikra fulani au tabia fulani ambayo
yeye haridhiki nayo. Ni muhimu kwa mwanaume vilevile kuzisoma tabia za
mke wake, vitu gani vinamuudhi, na vitu gani vinamfurahisha.
Katika ujenzi wa ndoa imara, kuna vigezo vingine
ambavyo si muhimu lakini havipaswi kupuuzwa, miongoni mwa vigezo hivyo
ni kiwango cha wanandoa kijamii na kiuchumi, hiki ni kigezo ambacho
kinaweza kuonekana ni cha kidunia zaidi, lakini uzoefu unaonyesha kuwa
kimekuwa ni miongoni mwa sababu zinazopelekea chokochoko katika familia
na hatimae kuikwaza ndoa yenyewe.
Inapotokea kwa mmoja miongoni mwa wanandoa hususan
mwanamume akawa na hali duni kiuchumi kuliko ile ya mkewe (familia ya
mkewe) basi pamoja na mapenzi yanayowaunganisha, maisha yao yatakuwa na
tahadhari kubwa sana, na wakati wowote kinaweza kutokea kitu ambacho
hakikutarajiwa na kikazua mtafuruku.Ni vema wanandoa wakaanza kujenga
misingi imara ya ndoa yao kwa kujitahidi kuzingatia kigezo hiki cha
Kiuchumi na Kijamii
Wapo watu wanaosema kwamba elimu siyo jambo la
msingi. Hata hivyo hilo siyo sahihi. Inapokuwa elimu ya mwanamke ni
kubwa kuliko ya mwanamume, kwa mfano, mwanamke anapokuwa na shahada ya
Chuo Kikuu, na mwanaume ya Darasa la Saba, hapa panahitaji hekima na
juhudi kubwa kwa mwanamke kuweza kumuelimisha mumewe bila ya kumfanya
ajihisi mjinga, zoezi ambalo ni gumu, na uwezekano wa kushindwa ni
mkubwa.
Aidha kuna suala la wanandoa kuishi karibu na
ndugu. Ndoa za ndugu wa karibu, zinaweza zikawa ni sababu ya kuimarika
kwa ndoa au sababu ya kudhoofika, lakini kwa uzoefu wetu imeonekana kuwa
ndoa za aina hii mara nyingi zinafikia katika hatua ya uzee mapema
zaidi, hii ni kutokana na kufahamiana kwa ndugu hawa tangu utotoni, na
kila mwanandoa kutotarajia jipya kutoka kwa mwenzake
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment