Home » » MUFTI SIMBA AWAHIMIZA WATANZANIAKUSHIRIKIANA,KUSAIDIANA KWA DHATI

MUFTI SIMBA AWAHIMIZA WATANZANIAKUSHIRIKIANA,KUSAIDIANA KWA DHATI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mufti wa Tanzania,Sheikh Mkuu, Issa bin Shaaban Simba
 
Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Issa bin Shaaban Simba, amewahimiza Watanzania kushirikiana na kusaidiana kwa hali na mali ndani ya jamii, ikiwamo kuwapatia elimu watoto wao.
Alitoa wito huo mjini Maswa, mkoani Simiyu, wakati akiongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kiilslamu ya Mhumbu, iliyoko eneo la Ugweto, Manispaa ya Shinyanga, inayomilikiwa na Waislamu.

Katika harambe hiyo, zaidi ya Sh. milioni tatu zilichangwa, zikiwamo fedha taslimu Sh. 1,096,000, ahadi Sh. milioni mbili na mifuko ya saruji 37.

Mufti Simba alisema Watanzania hawana budi kusaidiana katika masuala muhimu, ambayo pia humpendeza Mwenyezi Mungu, ambaye katika vitabu vyake vyote vitakatifu na mahubiri ya mitume wake wamehimiza elimu itafutwe popote na hata kama ni China.

Aliwataka watu kuwa na tabia ya kupenda kujitoa kwa kutenda mambo mema kwa wenzao kwanza na kuepuka tabia ya ubinafsi, uchoyo na kuwa kujitoa kwa mema Mungu humwongezea thawabu mja wake na kuwataka kuacha tabia ya kuombaomba bila kujitoa kwanza na kuwa mfano.

Akizungumzia ujenzi wa shule hiyo, alisema licha ya kuwa inajengwa mjini Shinyanga, bado itapokea na kutoa elimu kwa watoto wote bila ubaguzi wowote wa dini, rangi na kabila lengo ikiwa ni jamii kupata elimu, ambalo hupendwa na Mwenyezi Mungu.

Aliitaka katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kubadili tabia na kuwa wa kwanza kujitoa zaidi kwa Mwenyezi Mungu kwa kutenda mema na kuwa watalipwa maradufu.

Pia amewataka waumini wa dini ya kiislamu kuacha tabia na matendo machafu ya kumuudhi Mungu, ikiwamo, ubinafsi, uchoyo, uasherati, ulevi na kuzifananisha tabia hizo ni sawa kula nyama ya mtu tena maiti.

Ujenzi wa shule hiyo unakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwamo kulipa fidia ya Sh. milioni 47 kwa watu waliopisha maeneo yao katika mradi huo.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa