Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MATUKIO ya ukatili
dhidi ya watoto, bado yameendelea kushika kasi kwenye maeneo mbalimbali
nchini ambapo katika Mkoa wa Simiyu, mtoto mwenye umri wa miaka 17 (jina
tunalihifadhi), mkazi wa Bariadi Mjini na mwanafunzi wa Shule ya Msingi
Bariadi, amejikuta akifungwa minyororo mikononi na miguuni kwa miezi
minne nyumbani kwa mganga wa kienyeji.
Mganga huyo amefahamika
kwa jina la Mdeli Msanja ambaye aliamua kufanya ukatili huo baada ya
wazazi wa mtoto huyo ambaye anamatatizo ya akili, kushindwa kumlipa pesa
za matibabu.
Akizungumzia tukio
hilo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Charles Mkumbo, alisema wazazi wa
mtoto huyo walikubaliana na mganga huyo kumlipa sh. 260,000 kama mtoto
wao atapatiwa matibabu na kupona.
"Pamoja na wazazi
kukubaliana na mganga husika, hali ya mtoto haikuweza kubadilika wala
kupata unafuu hivyo waliomba kumchukua mtoto wao kitendo ambacho
kilipingwa na mganga kwa madai ya kutolipwa pesa zake ambazo
walikubaliana," alisema.
Alisema mganga huyo
aliamua kumchukua mtoto huyo na kumfungia chumbani kwake kwa minyororo
miguuni na mikononi kwa kipindi cha miezi minne akidai pesa zake na
kuwapa wakati mgumu wazazi wake.
Kutokana na msimamo wa
mganga huyo, mama mzazi wa mtoto huyo Malita James (46), alilazimika
kwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Bariadi kuhusu mateso anayoyapata
mwanaye kwa mganga.
"Polisi walishirikiana
na Dawati la Jinsia kufanya uchunguzi wa tukio hili na walipofika kwa
mganga, walimkuta akiwa amemfunga minyororo miguuni na mikononi,"
alisema Kamanda Mkumbo.
Aliongeza kuwa, polisi
walimkamata mganga huyo ambaye hakuwa na kibali cha kutoa tiba za asili,
pia alikamatwa na nyara za Serikali ambazo ni pembe moja ya swala na
mikia miwili ya nyumbu ambapo uchunguzi ukikamilika atafikishwa
mahakamani.
0 comments:
Post a Comment