Home » » WAFUASI WA CCM WAWASHAMBULIA CHADEAMA MEATU

WAFUASI WA CCM WAWASHAMBULIA CHADEAMA MEATU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Na Samwel Mwanga-Meatu.
WAFUASI wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)wilayani Meatu mkoani Simiyu juzi
waliwashambulia kwa mawe Wafuasi wa CHADEMA     waliokuwa wakifanya
maandalizi ya Mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Jimbo la Meatu,Meshack
Opulukwa(CHADEMA) katika uwanja wa Stendi mjini Mwanhuzi.
Tukio hilo lililotokea majira ya saa 5:30 asubuhi lilizua taharuki na
hivyo kusababisha shughuli mbalimbali zilizokuwa zikifanyika katika
eneo hilo na eneo la soko la Mwanhuzi kusimama kwa muda wa dakika 30
hadi hapo polisi walipofika na tuliza vurugu hizo.
Watu walioshuhudia tukio hilo waliwaeleza waandishi wa habari kuwa
wafuasi wa CHADEMA walikuwa wakipamba jukwaa la kuhutubia lililokuwa
katika uwanja huo ambalo ni mali ya Halmashauri ya Wilaya.
Mara walifika wafuasi wa CCM wapatao 20 na kuwataka wafuasi wa CHADEMA
wasiende na kazi hiyo kwani hapo ni eneo ambalo diwani wa Kata ya
Mwanhuzi mjini,Elia Shukia (CCM)analitumia kuonyeshea Runinga
mashindano ya soka ya  Kombe la Dunia.
“Hilo eneo ambalo ndilo tunafanyia mikutano yote ya hadhara mjini
Mwanhuzi kuna jukwaa ambalo ni mali ya Halmashauri wakati CHADEMA
wakiendelea kulipamba walivamiwa na wafuasi wa CCM na kuwataka
kuondoka mara moja kwani eneo hilo kwa sasa linamiikiwa na Diwani
Shukia(CCM)na wenyewe wakagoma”Alisema John Ndago.
Waliendelea kueleza kuwa baada ya mabishano yaliyochukua takribani
dakika tano na kushindwa kuelewana ndipo wafuasi wa CCM walianza
kuwashabulia wafuasi CHADEMA kwa kuwapiga kwa kutumia mawe,nondo na
fimbo.
Vurugu hizo ziliendelea kuwa kubwa baada ya  wafuasi wa CHADEMA kujibu
mapigo huku wakisaidiwa na baadhi ya wananchi kabla ya kutulizwa na
Askari polisi kutoka kituo cha wilaya waliofika katika eneo hilo .
Pamoja na Askari Polisi kutuliza vurugu hizo lakini ziliendelea ndipo
askari wa kikosi cha kuzuia Ghasia (FFU)kutoka mkoa wa Simiyu
walipowasili mjini humo na kuthibiti hali hiyo.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia baadhi ya wafuasi wa vyama hivyo
wakiwa wanavuja damu sehemu mbalimbali za miili yao baada ya kupigwa
na mawe.
Inadaiwa vurugu hizo zilikuwa zimeandaliwa na baadhi ya viongozi wa
CCM wilayani Meatu akiwemo diwani Diwani wa Kata ya Mwanhuzi,Elia
Shukia kwa lengo la kuzuia mkutano huo usifanyike.
 
Akizungumzia vurugu hizo Mlezi wa CHADEMA wilayani humo,Zacharia
Maghembe alisema kuwa chama hicho kimesikitishwa na kitendo hicho cha
wafuasi wa CCM kuwavamia wafuasi wao na kulitaka Jeshi la Polisi
kuchukua hatua kali kwa wahusika vinginevyo sasa wamechoka kuvumilia
vitendo hivyo.
“Kitendo kilichofanywa na wenzetu wa CCM wa kuwavamia wafuasi wetu
waliokuwa wakifanya maandalizi ya mkutano hakivumiliwi tunalitaka
jeshi la polisi kuwakamata wote waliofanya vitendo hivyo kwani
tunawafahamu kinyume cha hapo tumechoka kuonewa tutajibu
mapigo”alisema Maghembe.
 
Mbunge wa Jimbo la Meatu,Meshack Opulukwa alilaani tukio hilo na
kusema hizo ni siasa za kihuni na za kizamani ambazo zinapaswa
kulaaniwa na wapenda maendeleo wote na kudai kuwa viongozi wote
wanaosimamia mipango hivyo hawataki kuongoza jamii.
Polisi wilayani humo wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo na hakuna
mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na vurugu hizo.
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa