Home » » WANANCHI WATAKA ULINZI KWA ALBINO

WANANCHI WATAKA ULINZI KWA ALBINO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Kuanza upya kujitokeza mauaji ya walemavu wa ngozi (Albino) mkoani Simiyu, kumesababisha wananchi kuomba Serikali kuwawekea ulinzi mkali walemavu hao ili waishi kwa amani.
Hatua hiyo inatokana na mauaji ya mkazi wa Kitongoji cha Chalala, Kijiji cha Gasuma, Kata ya Mwaubigi, wilayani Bariadi, Munghu Lugata (40) kuuawa kikatili kwa kukatwa viungo vyake.
Wananchi waliojitokeza kwenye mazishi ya Lugata juzi, walisema walemavu wa ngozi wanatakiwa wasiishi peke yao, bali wakae na watu wengine ili kulinda usalama wa. Mwanamke huyo alikuwa akiishi na mtoto mdogo.
Dada wa marehemu, Minza Lugata alisema siku ya tukio baada ya kuamka asubuhi, walishangaa kuona mdogo wake amechelewa kuamka kwani haikuwa kawaida yake, hivyo walikwenda kugonga mlango na kukuta ukiwa wazi, walipoiniga ndani wakabaini ameuawa.
Lugata alisema walipiga yowe na majirani wakakusanyika, hatimaye kutoa taarifa kwa uongozi wa Serikali.
Alisema mdogo wake alikuwa amekatwa mguu wa kushoto kuanzia kwenye goti, amekatwa vidole vitatu vya mkono wa kushoto na kunyofolewa kucha la dole gumba.
“Dada yangu amekufa kifo kibaya, bora wangemkata wakamuachia uhai kwani amefariki akiwa tayari ana mimba ya mienzi mitatu, waliofanya hivyo hawana utu kabisa,” alisema Lugata.
Uongozi kijiji wanena
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Gasuma, Joshua Mussa alisema kwa zaidi ya miaka mitatu mwanamke huyo alikuwa akiishi peke yake na kwamba, aliwahi kuolewa na mwanaume ambaye ni vigumu kumtambu kwani alikuwa akionekana mara chache.
Mussa alisema mwanamke huyo alikuwa akiishi vizuri na familia, hawakuwahi kusikia migogoro na mumewe waliachana kwa amani.
Aliwataka walemavu hao wanaoishi peke yao, wapewe ulinzi na ndugu zao lakini Serikali inatakiwa kuwaandalia mazingira mazuri.
Naye Diwani wa Viti Maalumu, Hellen Ndibata alisema mauaji yalikuwa yametulia, hali iliyosababisha Serikali kujisahau matokeo yake yameanza upya.

Ndibata alisema Serikali inatakiwa kuweka mikakati mahsusi kwa kuwaandalia mazingira mazuri walemavu hao, kwa kuwaweka kambini kama walivyofanya kwa wanafunzi albino.
“Mauaji haya yalionekana kuisha hasa kanda yetu ya ziwa, mwaka huu yanaonekana kuanza upya, ni kazi sasa ya polisi kuhakikisha watu wanaojihusisha na biashara ya viungo vya albino wanakamatwa,” alisema.
Wawili mbaroni kwa mauaji
Polisi inaendelea kuwashikilia watuhumiwa wawili ambao ni waganga wa jadi na kwamba, msako zaidi unaendelea kwa wengine waliohusika.
Kamanda wa Poilisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo alisema hadi jana walikuwa akiwashikilia waganga hao wa jadi.
“Mganga mmoja kwa mujibu wa ndugu, awali marehemu alimtuma mtoto mdogo kwenda kwa mganga huyo kuchukua dawa, kwani marehemu alikuwa akijisikia homa baada ya kufika mtoto huyo kwa mganga alimweleza shida aliyokuwa ametumwa,” alisema Mkuombo na kuongeza:
“Mganga akamweleza kuwa sema imeisha, lakini akamwambia leo usilale nyumbani uende kwa mama mkubwa wako, mtoto huyo hakujua kinachoendelea mpaka mwanamke huyo alipouawa.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa