Home » » NUKSI ZA WAPAMBE NUKSI

NUKSI ZA WAPAMBE NUKSI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Na Richard Mabala

Katika karne ya kumi na tisa, kulikuwa na mwandishi mmoja wa Urusi aitwaye Tolstoy. Aliandika riwaya bora sana, pia alikuwa mwanafalsafa aliyependa sana usawa, ingawa yeye mwenyewe tajiri na aliyechukia sana matumizi yoyote ya nguvu na ukatili.
Kutokana na umaarufu wake, alipata wafuasi wengi. Sasa kichekesho ni kwamba hatimaye wafuasi walikuwa na nguvu kuliko Tolstoy mwenyewe, hasa pale alipoanza kuzeeka.
Hivyo, walichambua kila alichoandika hata kabla hakijachapishwa kisha kukibadilisha, eti kinaenda kinyume na Utolstoy wake. Yeye ndiye Tolstoy, lakini wao waling’ang’ania kufinya utolstoy wake hadi ufanane na walichotaka wao. Na waliweza kufanya hivyo kwa sababu walikaa kwake, walikula kwake na kufaidi matokeo yote ya uandishi bora wa Tolstoy.
Mwishowe Tolstoy wa watu akiwa na takriban miaka tisini, alilazimika kujaribu kutoroka nyumbani kwake ili apate uhuru. Alitoroka usiku na kufanikiwa kufika mbali kidogo, lakini afya yake ikamsaliti, akaugua na ikabidi arudishwe nyumbani na kufariki muda mfupi baadaye.
Hapo sasa. Hata sisi wengine tunabadilika na kuwa na mawazo na misimamo mipya kidogokidogo kutokana na kusoma zaidi, kujadili zaidi na kupata mikasa na uzoefu mbalimbali katika maisha yetu na kama tuko tayari kutumia akili yetu, hasa kutafakari kuhusu hayo yote tuliyosoma, kujadili na kupitia. Na iwapo ni hivyo kwetu, nadhani ni zaidi kwa watu ambao umaarufu wao unatokana na kutafakari zaidi, kusoma zaidi, kupata uzoefu zaidi na kadhalika. Utamfinyaje mtu kama huyu badala ya kumwachia aendelee kutafakari kwa kina zaidi na kuona mengine ambayo yanaweza kutufikirisha zaidi?
Tutamlaanije mtu, eti amebadili mawazo kama vile kubadili mawazo ni kufisadi au kuua? Kubadili mawazo ni sehemu ya ubinadamu wetu na ingawa wengine wanabadili kutokana na pochi tu, siyo haki kumshambulia kila mtu aliyebadilika kwa kuwa pochi imetawala. Hata kutobadili mawazo kunaweza kutokana na pochi pia.
Nadhani ndiyo maana Waswahili hupenda kusema ‘wapambe nuksi’. Licha ya mambo mengine ya kujipendekeza na kutaka kumfaidi mtu, wao daima wanapamba ya jana wakati mtu ameshasonga mbele zaidi leo. Akitaka kusonga mbele zaidi, wanamvuta nyuma ili afuate yayo hayo. Hii ndiyo maana ya uhafidhina wa kijinga. Dunia inabadilika, lakini wanataka sote tugande kama vile tuko katika friza. Mwisho wa mawazo mgando ni kifo cha mawazo.
Naam, najua wengine watamcheka Tolstoy aliwezaje kutawaliwa hivyo na kushangaa wale waliomfinya kwa kujidai ni wajuzi kuliko yeye, lakini mbona sisi tunafanya vilevile. Angalia wapambe nuksi wa dini ambao wako tayari kuchukua neno moja la waanzilishi wa dini zao na kulitumia kuwaangamiza watu wengine huku neno hili likigongana kabisa na maneno elfu yenye wazo tofauti.
Tunachukua yale tu ambayo tunayataka sisi. Ndiyo maana wengine wanasema si kweli Mungu alituumba kwa mfano wake. Sisi wapambe nuksi tunamwumba (na kumwumbua!) kwa mfano wetu.
Kwa nini naongelea yote hayo? Nimesoma habari ambazo siwezi kuziamini. Siwezi kuamini kwamba, licha ya kujaribu kufinya maneno na busara hai ya baba wetu wa taifa, watu wanataka kumfinya na kumtia kwenye friza kama vile hakubadilika na yeye. Na sasa wanathubutu kumfinya hata mjane wake.
Nani anaweza kusahau wakati wa kufariki kwa baba yetu, jinsi alivyoagwa na wananchi wake hadi alipozikwa? Lakini katika kumbukumbu zangu zote, kuna moja ambayo inanigusa hadi moyoni kila nikiifikiria.
Baada ya watu wote kumaliza vyao, namkumbuka Mama Maria akienda huko kaburini ambapo tayari ilikuwa imefunikwa. Akapiga magoti mbele yake na kutandaza mkono wake juu ya kaburi. Kilikuwa ni kitendo kidogo, lakini kitendo kilichobeba maana pana na ya kina kabisa.
Hicho kitendo kilibeba maumivu yake yote ya kumkosa mwenzake, pamoja na mshikamano wake naye hadi kaburini. Mtu aliyeona hilo aliweza kuhisi ukaribu wa mama na baba. Waliishi pamoja, waligawana maoni yao, walijitolea kujenga taifa badala ya tumbo, hadi kweli wakawa wamoja kwa namna ambayo simenti ya kaburi haiwezi kabisa kuwatenganisha.
Wanaosoma makala zangu wanajua kwamba siyo kawaida yangu kutaja jina la mtu, lakini leo sina budi kufanya hivyo maana ninamheshimu Mama Maria kupita kiasi.
Sote tunajua kwamba yeye siyo msemaji sana ndiyo maana akisema, tunatega sikio kwa nguvu zote, maana maneno yake ni tunu kwetu.
Sasa, alichosema juzi kuhusu mustakabali wa taifa letu siyo la kupuuza hata kidogo. Ndipo hapo tunaingia kwenye mambo ya wafuasi wa Tolstoy. Wapambe nuksi watakana alichosema na kujaribu kuponda na hata kuficha alichokisema, lakini maneno yake ni hai kuliko yao.
Halafu bado siamini, yaani haiingii akilini, lakini sijaona anayekanusha, eti mama yetu wa taifa anaamriwa asome magazeti hadi analazimika kumtuma mtu kupata magazeti anayotaka yeye, lakini ambayo wapambenuksi hawataki aone. Hivi kuna ujinga zaidi ya huu? Kuna udhalilishaji zaidi ya huu? Kuna ukiukwaji wa haki za watu kuliko huo? Tena kwa mama wa taifa.
Lakini la kushangaza ni kwamba hata magazeti hawajaamka na kulaani vikali kunyimwa kwake haki ya kupata taarifa. Hivi ni wapambe nuksi na wao au wamefinywa? Mbona hakuna ufuatiliaji? Ingekuwa Makengeza amenyimwa magazeti sawa, lakini Mama wa Taifa? Haiyumkiniki.
Hata hivyo, imenikumbusha jinsi ofisi zetu zinavyopambwa na magazeti ambayo sisi tulio wengi hatusomi. Sijui ni katika mkataba kwamba lazima waweke gazeti la Serikali na la chama tawala tu, lakini sielewi sababu yake. Msingi wa demokrasia siyo kufinya mawazo ya watu bali kupanua, ila iwapo lengo ni kufanya watu wasinzie wakati wanasubiri basi wamefanikiwa sana.
Hivyo, siwezi kumshauri mama yetu naye ajaribu kutoroka kama Tolstoy, lakini nadhani ni muhimu sana tuhakikishe kwamba yeye, pamoja na sisi sote wengine tunapata habari za uhakika, tunapata haki yetu ya kusoma vyanzo mbalimbali ili tuweze kutumia akili yetu kuchambua.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa