Home » » ALBINO AUAWA KINYAMA,ANYOFOLEWA VIUNGO VYAKE

ALBINO AUAWA KINYAMA,ANYOFOLEWA VIUNGO VYAKE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu,Charles Mkumbo
 
Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yaliyoibuka kwa kasi katika baadhi ya mikoa ya kanda ya Ziwa miaka ya hivi karibuni, yameibuka tena baada ya mwanamke mmoja kuuawa mkoani Simiyu na wauaji kuondoka na baadhi ya viungo vya mwili wake.
Tukio hilo lilitokea katika kitongoji cha Mwachalala, kijiji cha Gasuma, Kata ya Mwaubingi, wilayani Bariadi usiku wa Mei 12, mwaka huu saa sita usiku.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu,Charles Mkumbo, jana aliliambia NIPASHE kuwa watu wasiojulikana walivamia nyumbani kwa marehemu, Munghu Lugota (40), na kumshambulia kwa kumkata sehemu mbalimbali za mwili na kuondoka na baadhi ya viungo vyake.

Kamanda Mkumbo alisema watu hao walimkata marehemu mguu wake wa kushoto kuanzia sehemu ya chini ya goti, vidole viwili vya mkono wa kushoto.

Kwa mujibu wa Kamanda Mkumbo, pia walimkata marehemu ukucha wa dole gumba la mkono wa kushoto na kutoweka navyo kusikojulikana.

Kamanda Mkumbo alisema kuwa kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi lilichukua hatua kwa kuanzisha msako mkali uliowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa wawili ambao wako mikononi mwa polisi.

Kamanda Mkumbo alisema kuwa watuhumiwa hao ni waganga wa jadi mmoja akiwa ni mpiga ramli mashuhuri kijijini hapo (majina tunayahifadhi kwa sasa).

Kamanda Mkumbo alisema kuwa siku ya tukio, kuna watu waliofika nyumbani kwa watuhumiwa hao.

Habari zinaeleza kuwa watu hao walifika nyumbani kwa waganga hao siku ya mauaji ya mwanamke huyo.

Kwa mujibu wa Kamanda Mkumbo, tayari kikosi maalum cha upelelezi kimenza kazi ya kuwasaka wauaji hao na aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi.

Kadhalika, Kamanda Mkumbo alitoa wito kwa wananchi wenye tamaa ya utajiri kondokana na imani za kishirikina kwa kuamini kuwa na kiungo cha binadamu hasa mwenye ulemavu wa ngozi ni kupata utajiri badala yake wafanye kazi halali kwa bidii.

Alisema kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi mkoani Simiyu linaomba ushirikiano wa raia wema kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za siri kwa jeshi hilo kwa lengo la kuwabaini watu wanojihusisha na mauaji hayo.

Kamanda Mkumbo aliwaomba wananchi kuwasiliana kwa namba 0754 380 176 ambayo ni ya Kamanda wa Polisi mkoa (RPC) Simiyu au 0754 894 032 ya Kamanda wa Upelelezi wa mkoa wa Simiyu (RCO) Simiyu au 0754 895 872 ya Mkuu wa Kitengo cha Itelijinsia mkoa wa Simiyu.

Kamanda huyo aliwahakikishia wananchi kwamba  taarifa zote zitatunzwa na hakuna siri itakayotolewa.

MAUAJI ALBINO 2010
Novemba mwaka jana Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki, alilimbia kuwa watuhumiwa wanane wa mauaji ya albino nchini walihukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya watu hao.

Kairuki alisema jumla ya matukio 60 ya mauaji na kujeruhiwa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi yameripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini tangu mwaka 2007 na kati ya hayo, 35 yalifikishwa mahakamani na watuhumiwa 25 hawajakamatwa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa