Na Samwel Mwanga-Maswa
MKUU wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu,Luteni Mstaafu Abdalah Kihato
amemshangaa Diwani wa Kata ya Zanzui wilayani humo,Jeremeah
Shigala(CCM)kwa kitendo cha Kata hiyo kutaka kujenga shule ya
sekondari ya kidato cha sita wakati hawana shule ya sekondari ya
kuanzia kidato cha kwanza.
Hali hiyo ilijitokeza jana katika kikao cha baraza la madiwani
kilichofanyika jana katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo mjini
Maswa wakati diwani huyo akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya Kata ya
Zanzui.
Akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya wajumbe wa baraza hilo alisema kuwa
Kata hiyo imejipanga kujenga shule maalum ya wasichana itakayokuwa na
kidato cha tano na sita na itajulikana kwa jina la Philipo Ndaki ikiwa
ni ahadi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
“Mheshimiwa Mwenyekiti katika Kata yetu ya Zanzui katika suala la
elimu tumejipanga vizuri kwanza tumeweka mkakati wa kujenga shule
maalum ya wasichana ya kidato cha tano hadi kidato cha sita
itakayoitwa Philipo Ndaki High School ikiwa ni ahadi ya aliyekuwa Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga,Dk Yohana Balele”alisema.
Alisema kuwa shule hiyo inatarajia kujengwa katika kijiji cha Malita
ikiwa ni kumbukumbu ya Philipo Ndaki aliyekuwa Mwenyekiti wa Vyama vya
Ushirika Tanzania.
Mara baada ya kumaliza kuwasilisha taarifa yake hiyo ambayo ilizua
minongono kwa baadhi ya wajumbe hao Mkuu wa Wilaya,Kihato alisimama na
kueleza mshangao wake kuwa inakuwaje waanze kujenga shule hiyo wakati
Kata hiyo haina shule ya sekondari ya kidato cha kwanza hadi cha nne.
“Mie nashangaa diwani hapa anatueleza ya kuwa wana mpango wa kujenga
High School wakati katika Kata yake hakuna hata shule ya sekondari ya
olevel na akumbuke hata wakijenga shule hiyo hawatakuwa na mamlaka
nayo itachukuliwa tu na serikali kuu kwani ndiyo mmiliki na
mwendeshaji wa shule hizo”alisema.
Kihato aliendelea kueleza kuwa ni vizuri wakajenga shule ya sekondari
ya kidato cha kwanza hadi cha nne kwani wanafunzi wanaomaliza elimu ya
msingi hujiunga na masomo ya kidato cha kwanza katika shule za Kata
jirani za Buchambi na Mwighwa ambazo ziko umbali wa kilomita 15 kutoka
katika Kata hiyo.
Kata hiyo imeshindwa kujenga shule ya sekondari ya kidato cha kwanza
hadi cha nne kwa kipindi kirefu huku diwani huyo akiishawishi
Halmashauri ya wilaya hiyo kununua shule ya sekondari ya mtu binafsi
iliyoko katika Kata ya Zanzui kwa gharama ya shilingi milioni 200
jambo ambalo limepingwa .
Home »
» MKUU WA WILAYA AMSHANGAA DIWANI
MKUU WA WILAYA AMSHANGAA DIWANI
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment