Na Samwel Mwanga-Meatu
MBUNGE wa jimbo la Kisesa(CCM)wilayani Meatu mkoani Simiyu,Luhaga
Mpina na Mkuu wa Wilaya hiyo,Rosemary Kirigini wametoa pikipiki 25
zenye thamani ya Shilingi Milioni 55 kwa Chama Cha
Mapinduzi(CCM)wilayani humo.
Sherehe za kukabidhi pikipiki hizo zilifanyika katika ukumbi wa
halmashauri ya wilaya hiyo uliko mjini Mwanhunzi na kuhudhuriwa na
viongozi mbalimbali wa chama hicho wilayani humo.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo Mbunge,Mpina alisema kuwa
pikipiki hizo zitagawiwa kwa Makatibu wa Kata wa CCM katika wilaya
hiyo kwa lengo la kuimarisha shughuli za chama.
“sisi tukiwa makada wa CCM kwa pamoja tumeamua kushirikiana kwa pamoja
na tukapata pikipiki hizi 25 kwa kila Kata zilizoko ndani ya wilaya
yetu hivyo tumeona tuwapatie Makatibu wa Kata ili tuboreshe utendaji
kazi wao na kuwarahisisha kupunguza umbali wa kila siku wanapokuwa
na majukumu ya kukiimarisha na kukijenga chama katika maeneo
yao”alisema.
Naye Mkuu wa wilaya hiyo,Kirigini ambaye pia ni Mbunge wa viti
Maalum(CCM)Mkoa wa Mara alisema kuwa ni vizuri pikipiki hizo
zikatumiwa kama zilivyokusudiwa na siyo kuzigeuza kufanyia biashara ya
kubebea abiria.
“Ni vizuri pikipiki hizi zikatumiwa kwa malengo yalivyokusudiwa na
isije mkazigeuza kuwa bodaboda huko katika maeneo yenu kufanya hivyo
mtakuwa hamjatutendea haki siye tulizozitafuta na kuwagawia pamoja na
CCM”Alisema.
Katibu wa CCM Kata ya Mwanhuzi,Mawazo Shabani kwa niaba ya wenzake
waliopata pikipiki hizo mbali na kuwapongeza viongozi hao alisema
kuwa sasa utendaji wa kazi zao utakuwa rahisi kwani wataweza kufika
maeneo yao kwa wakati ha kuhaidi kuzitumia pikipiki hizo kwa malengo
yaliyokusudiwa.
Diwani wa Kata ya Mwanhuzi,Eliya Shukia akiongea kwa niaba ya CCM
Wilayani humo pia aliwashukuru viongozi hao kwa kitendo walichokifanya
na kueleza kuwa huo ni mwanzo mzuri wa chama hicho kuelekea katika
uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu unatarajia
kufanyika mwakani.
Wilaya ya Meatu inazo kata 25 na majimbo mawili ya uchaguzi mojawapo
likiwa jimbo la Kisesa linaloongozwa na Luhaga Mpina(CCM) na Jimbo la
Meatu linaloongozwa na Meshack Opulukwa(Chadema).
Simiyu yetu Blog
0 comments:
Post a Comment