Home » » NEWS ALERT: VIFO AJALI YA BASI LA LUHUYE VYAONGEZEKA NA KUFIKIA 15

NEWS ALERT: VIFO AJALI YA BASI LA LUHUYE VYAONGEZEKA NA KUFIKIA 15

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 

 

 
Na Samwel Mwanga-Simiyu
 
IDADI ya vifo vilivyotokea kufuatia ajali mbaya ya basi la Luhuye
Express linalofanya safari zake kati ya mji wa Tarime mkoani Mara na
Jijini Mwanza iliyotokea April 21 mwaka huu majira ya saa 5:11 asubuhi
 katika kijiji cha Itwimila wilayani Busega mkoa wa Simiyu imeongezeka
na kufikia 15.
 
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu,Kamishina
Mwandamizi wa Polisi(SACP),Charles Mkumbo kwa vyombo vya habari
inaeleza kuwa idadi hiyo imeongezeka kufuatia kufariki kwa majeruhi
wanne wa ajali hiyo waliokuwa wakipatiwa matibabu katika hospitali ya
Rufaa ya Bugando.
 
Kamanda Mkumbo aliwataja marehemu ambao hadi sasa wametambuliwa kuwa
ni Mohama Kidela(32) mkazi wa Bugarika Jijini Mwanza,Alex
Masatu(42)mkazi wa Musoma,Wangwe Morice(30) Afisa Elimu Msaidizi
Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Mahemba Chacha(42)mkazi wa
Serengeti mkoani Mara,Thomas Mwita(40)ambaye ni Mchungaji wa kanisa la
SDA mjini Kahama mkoani Shinyanga.
 
Wengine ni pamoja na Esther Morice(18) mkazi wa Tarime mkoani
Mara,Rose Willison(21) mkazi wa Igoma Jijini Mwanza,Shepa Msongoma(58)
mkazi wa Nassa wilayani Busega na Mtoto Baarka Alex(1) ambaye makazi
yake hayajajulikana.
 
Pia Kamanda Mkumbo amewaomba watu mbalimbali kufika katika hospitali
ya Rufaa ya Bugando  Jijini Mwanza  ili kuweza kutambua miili ya ndugu
zao kwani hadi sasa maiti sita bado hazijatambuliwa.
 
Majeruhi 33 bado wanaendelea na matibabu katika hospitali ya Bugando
Jijini Mwanza na majeruhi 11 bado wanaendelea na matibabu katika
hospitali ya wilaya ya Magu mkoani Mwanza.
 
Katika hatua nyingine jeshi la polisi mkoani humu linamshikilia
mmiliki wa basi hilo,Masalu Jackson mkazi wa Majengo mjini Bunda
mkoani Mara ambaye alikamatwa wilayani Busega mkoani humu kufuatia
ushirikiano wa jeshi la polisi na wananchi huku wakiendelea kumtafuta
aliyekuwa dereva wa Basi hilo ambaye jina lake halijapatikana
alitoroka mara baada ya ajali kutokea.
 
Basi la Luhuye Express lenye namba za usajiri T 410 AWQ liliacha njia
na kugonga nyumba ya marehemu Mwalimu,Lazaro Mbofu na kuibomoa yote na
kisha kupinduka na watu 10 kufa papo hapo.

  Geita yetu Blog

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa