Na Samwel Mwanga-Maswa MKUU wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu,Luteni Mstaafu Abdalah Kihato amezindua wiki ya chanjo jana katika halmashauri ya wilaya hiyo na kuwahimiza wananchi kuona umuhimu wa kuwapeleka watoto wote kupata chanjo wanazostahili. Uzinduzi huo ambao ulihudhuriwa na wananchi wachache umefanyika katika zahanati ya Malita kata ya Zanzui kwa kuzindua chanjo za kuhara(Rotavirus)na Nimonia(PCV 13) kwa watoto wa chini ya mwaka mmoja. Alisema kuwa chanjo iliyokamilika ndiyo msingi wa kuwa na afya njema kwa sababu mwili utakuwa na kinga ya maradhi kwa miaka mingi. “Watoto ni binadamu dhaifu sana wanahitaji uangalizi wa karibu na wa hali ya juu sana maana katika maisha yao hawana wanachokijua isipokuwa titi la mama kwa hiyo wanahitaji sana huduma ya chanjo iliyokamilika ili waishi na kuimarika kwa afya zao”alisema. Pia amewataka wazazi kuwapeleka watoto wao kwenye vituo husika ili kupatiwa chanjo hizo huku akiwataka kutoa taarifa endapo muuguzi yeyote atawatoza fedha wakati wa chanjo hizo kwani zinatolewa bila malipo yoyote. Awali mganga Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dr Jonathan Budenu alisema kuwa kiwango cha ufanisi kwa chanjo ya Pentavalent 3 inayozuia magonjwa matano ambayo ni Kifaduro,Dondakoo,Pepopunda,Homa ya Ini na Homa ya Uti wa mgongo kimeongezeka kutoka asilimia 82 mwaka 2012 hadi asilimia 93 mwaka 2013. “Katika wilaya yetu ya Maswa kiwango cha ufanisi kwa chanjo ya Pentavalent 3 kimeongezeka kwani mwaka 2012 hadi 2013 watoto 18,481 walichanjwa kati ya watoto 19,807 na hawa chini ya umri wa miaka mitano”alisema. Dr Budenu pia alieleza kuwa wamekuwa wakipambana na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa zoezi hilo ambazo ni pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu umuhimu na ukamilishaji wa chanjo zote,watoto wapatao 1326 hawakupata au kukamilisha chanjo na ukosefu wa usafiri kwa ajili za kliniki za mkoba za chanjo kwa baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya. Ujumbe wa Wiki ya Chanjo wa mwaka huu ni Jamii iliyokamilisha chanjo ni jamii yenye afya wenye kauli mbiu isemayo”Chanjo ni jukumu letu sote”.
Home »
» DC MASWA AZINDUA WIKI YA CHANJO
DC MASWA AZINDUA WIKI YA CHANJO
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment