WALIMU wa shule za msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa,
mkoani Simiyu, wamemtaka mkurugenzi na mwenyekiti wa halmashauri hiyo
kumwondoa Ofisa Elimu wa Shule za Msingi wilayani humo, Mabeyo Bujimu
kwa madai ya kuwa kikwazo katika utendaji kazi wa idara hiyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Maswa jana, walimu hao
walisema wameamua kuchukua uamuzi huo kutokana na tuhuma mbalimbali
zinazomkabili ofisa huyo, kwani wamebaini vitendo anavyofanya vinaweza
kukwamisha mikakati iliyowekwa na wilaya hiyo kuinua taaluma.
Walisema amekuwa akitumia lugha chafu kwa walimu huku akiwatishia,
hasa walimu wanaofundisha maeneo ya mjini kuwa atawahamishia shule za
vijijini, hali inayotoa tafsiri kuwa wanaofundisha vijijini ni kama
wamepewa adhabu.
“Huyu Ofisa Elimu amekuwa akitembelea katika shule na kututisha sisi
walimu kuwa atatuhamishia shule za vijijini, na hivi karibuni alifuta
kwa mdomo uhamisho wa mwalimu Hadija Shwaibu aliyekuwa amehamishiwa
Shule ya Msingi Nghami na kumrejesha Shule ya Msingi Hinduki huku
akimtuhumu Ofisa Elimu Taaluma, Patrick Musira alipokea rushwa na kutoa
uhamisho huo jambo ambalo si kweli,” alisema Said Juma.
Pia walimtupia lawama kwa kutumia nafasi yake kuwataka kimapenzi walimu wa kike sambamba na kuwateua kwa upendeleo.
Walisema mbali na tuhuma hizo amekuwa akitumia vibaya gari la idara lenye namba za usajili SM 4708.
Mbali na hayo walilalamikia kitendo cha kutoa amri kwa walimu wa
Shule ya Msingi Binza kuwazomea walimu wa Shule ya Msingi Shanwa kwa
madai kuwa hawakufanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa darasa la
saba mwaka jana, hali ambayo imewavunja moyo walimu waliozomewa.
Akizungumzia tuhuma hizo, Ofisa Elimu huyo, Mabeyo alisema anafahamu
chanzo cha malalamiko hayo kinatokana na kusitisha uhamisho wa baadhi
ya walimu bila barua, ambao anadai ulitolewa kinyemela na maofisa
wenzake.
Hata hivyo, alipotakiwa kuyatolea ufafanuzi malalamiko mengine,
alikataa hadi atakapowasiliana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Maswa, Hilda Lauwo.
“Haya malalamiko yote na hata kuitwa kwa waandishi wa habari kunihoji
hapa kunatokana na mimi kusitisha uhamisho kwa baadhi ya walimu
waliopewa uhamisho kinyemela kutoka ofisini kwangu, haya mengine labda
niwasiliane na mkurugenzi, akikubali basi nitayajibu na kuyatolea
ufafanuzi mbele ya wenzangu,” alisema.
Hata hivyo, alipotakiwa na waandishi wa habari kujibu tuhuma
zinazomhusu yeye mwenyewe kama vile kuwa na mahusiano ya kimapenzi na
walimu wa kike kwa kutumia madaraka yake, alipata kigugumizi na
kusisitiza kuwa hadi aonane na mkurugenzi.
Chanzo; Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment