Home » » WAJUMBE WA BARAZA LA MAMLAKA YA MJI MDOGO WASTUKIA MAPIPA YA TAKA

WAJUMBE WA BARAZA LA MAMLAKA YA MJI MDOGO WASTUKIA MAPIPA YA TAKA



 
Na Samwel Mwanga- Simiyu.
 
WAJUMBE wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Maswa katika mkoa wa Simiyu
wameyakataa mapipa ya taka ngumu yaliyoagizwa na mamlaka hiyo kwa
madai hayafai kuuweka mji huo katika mazingira ya safi.
 
Katika hali ambayo imeonyesha kuwepo harufu ya ufisadi juu ya mpango
wa ununuzi wa mapipa hayo yapatayo 20,wajumbe kwa kauli moja juzi
walipinga ununuzi wa mapipa hayo ambayo licha ya kuwa yameisha
nunuliwa tayari, lakini hadi sasa wajumbe hawajui yana thamani gani.
 
Akiwasilisha taarifa ya kamati ya elimu,afya na maji ya mamlaka hiyo
mbele ya wajumbe wa kikao hicho kilicho keti mjini Maswa, Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Caroiline Shayo alisema,jumla ya mapipa 20
yamenunuliwa na kamati yake haijui yanathamani gani licha ya kutojua
ubora wake kwa kuuweka mji huo mdogo katika hali ya usafi na mazingira
yake.
 
Wakichangia hoja juu ya kukataliwa kwa mapipa hayo, ambayo
hayakutangazwa katika zabuni yoyote kwa mujibu sheria ya manunuzi ya
umma,mmoja wa wajumbe hao Ziada Hamis, diwani wa viti maalum
alisema,licha ya kutojua yameigaharimu mamlaka hiyo shilingi ngapi
lakini pia kwa waliyo yaona wanadai hayafai kwa kukusanya taka ngumu
zinazo zalishwa ndani ya mamlaka hiyo.
 
Katika kikao hicho wajumbe walihoji iweje mapipa hayo yanunuliwe bila
kufuata taratibu za sheria ya manunuzi ya umma,huku wajumbe wengi
wakidai hawajayaona wala kuiona sampuli ya mapipa hayo.
 
Katika taarifa yake kaimu Afisa Afya, Ahmed Makono alisema, mapipa hayo
 ni kwa ajili ya kukusanya taka ngumu zikiwemo karatasi za vocha
zinazokwanguliwa na wateja wa simu za kiganjani, na taka zingine ngumu
kutoka majumbani na maeno mitaani.
 
Makamu mwenyekiti wa Mamlaka hiyo ,Hassan Tindo alisema wameshangazwa
na ununuzi wa mapipa hayo ambayo alidai hayaendani na hali halisi ya
mazingira na usafi wa mji huo ambao unakadiriwa kuwa na zaidi ya kaya
5000,katika kata za Nyalikungu na Binza.
 
Alipohojiwa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Maswa
Salima Mahizi, ambaye pia ndiye Afisa Afya wa mamlaka ya mji
huo,alikiri kuwepo kwa mapipa hayo, lakini alikataa katakata
kuzungumzia kwa kina juu ya ubora,thamani na taratibu zilizotumika
kuyanunua mapipa hayo,huku akisisitiza kuwa anayepaswa kuyasemea ni
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa.
 
Afisa huyo ambaye alikuwa katibu wa kikao cha baraza hilo
alisema,uamuzi wa kununua mapipa hayo ulifikiwa wakati wa ziara ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete, mwishoni mwa
mwezi Novemba mwaka jana, kwa lengo la wageni kuuona mji wa Maswa kuwa
ni safi.
 
Hata hivyo tangu ziara ya rais Kikwete ya siku saba kumalizika desemba
2013,hadi sasa hakuna pipa hata moja la taka lilowekwa mitaani kwa
lengo la kukusanya taka ngumu, na taka za mamlaka za mji huo zimekuwa
zikitupwa ovyo na kusababisha baadhi ya maeneo kuwa machafu na kutoa
harufu kali.
 
Aidha Mahizi alipohojiwa waandishi wa habari  alidai anasubiri maelekezo ya
kiongozi wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halamshauri ya Wilaya ya
Maswa,hata hivyo licha kuwa yeye ni Afisa Afya wa Mji huo ,alishindwa
kueleza ni kiasi gani cha taka ngumu kinachozalishwa katika mamlaka
hiyo, na ni maeneo gani mapipa hayo yamaelengwa kuwekwa, katika
mamlaka ya mji huo ambayo imekuwa moja ya mji ina historia ya kukumbwa
ugonjwa hatari wa kipindupindu.
 
Baadhi ya wajumbe walisema kuwa lengo la kuwepo kwa mapipa ya taka
ngumu ilikuwa ni kuuweka mji katika mazingira safi kwa kusanya taka
katika maeno ya Biafra,Nyalikungu na Kituo kipya cha mabasi kabla
trekta linazoa taka na kuzitupa dampo lililoko barabara ya Maswa
kuelekea Shinyanga.
 
Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa maeneo ya Biafra na Nyalikugu
Biafra Mariamu Juma alisema ,mji huo unapaswa kuwa na mikakati mizuri
ya kuuweka safi kwa vile una lengo la kuwa moja ya halmashauri ya mji
katika mkoa wa Simiyu.
 
Juhudi za kumpata Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Maswa Hilda
Lauwo,kwa njia ya simu zake za kiganjani haikuzaa matunda pale simu
hizo zilipo jibu mara zote "Mtumiaji wa simu unaye mpigia
hapatikani...." na hadi tunakwenda mitamboni hakupatikana.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa