MKOA WA SIMIYU UNATISHA KWA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU
Na Samwel Mwanga-Simiyu.
MKOA Wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa sita nchini ambayo inakabiliwa
na maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama Mjamzito
kwenda kwa mtoto.
Hayo yamelezwa jana na Dr Hamis Kulemba ambaye ni Mratibu wa kuzuia
magonjwa ya ngono na Ukimwi mkoa wa Simiyu wakati wa sherehe za
uzinduzi wa mpango wa kutokomeza maambukizi mapya ya VVU kwa mtoto
kutoka kwa mama mkoani humu katika viwanja wa Sabasaba mjini Bariadi.
Dr Kulemba alisema mpango huo ni mwitikio wa mpango wa kitaifa wa
utokomeza VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kutoka asilimia 15 ya
mwaka 2012 hadi kufikia chini ya asilimia nne ifikapo 2015.
Alisema mpango huo unalenga kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa
asiliami 50 miongoni mwa wanawake wenye umri wa kuzaa kati ya miaka
15 hadi 49 na kuongeza na kuboresha upatikanaji wa huduma za uzazi wa
mpango miongoni mwa akina mama wenye maambukizi ya VVU.
"Aidha mpango huu utaongeza upatikanaji wa tiba ya ARV kwa akina mama
wajawazito na wanaonyonyesha na kwa watoto walioambukizwa VVU,"
alisema.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Dr Matoke Muyenjwa alisema
kwa kupitia mpango huo akina mama wajawazito na watoto wote
walioambukizwa VVU wataanzishiwa dawa za ARV ambazo wataendelea
kuzitumia kwa maisha yao yote.
Alisema mpango wa kutoa dawa za kuzuia maambukizi ya VVU uanze,
maambukizi ya VVU toka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto yanapungua
mwaka hadi mwaka.
'huduma ya kuzuia maambukizi toka kwa Mama kwenda kwa mtoto iliendelea
katika wilaya zote mkoani hapa kati ya Januari, 2013 hadi Septemba,
2013 akina mama wajawazito 36,966 walipimwa VVU ambapo kati yao
wajawazito 701 walionekana na VVU sawa na asilimia 2 watoto
waliozaliwa na mama wenye maambukizi ya VVU walikuwa 895 na kati ya
hao watoto 66 sawa na asilimia 7.3 waligundulika kuwa na maambukizi ya
VVU'alisema. .
Aliongeza kueleza kuwa wanawake wajawazito wakijifungulia kwenye vituo
vya kutolea huduma serikali itawahakikishia usalama na watapewa elimu
ya namna ya kuzuia maambukizi kwa mtoto na sasa wana vituo 34 kati ya
mahitaji ya vituo 135.
Akizindua mpango huo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Paschal Mabiti katika
hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa wilaya ya Itilima,Bi Geogea Bundala
aliwataka wanaume kutowapuuza wenzi wao wanapokuwa katika kipindi cha
ujauzito na kuambatana nao kliniki ili kupata ushauri wa pamoja kwa
ajili ya kulinda afya zao na afya ya mtoto anayetarajiwa kuzaliwa.
Alisema utafiti unaonesha idadi kubwa ya waume wanapuuza kuambatana na
wenzi wao wakati wa mahudhurio ya kliniki sababu kubwa ikiwa ni woga
wa kujua hali ya afya zao na aibu.
"Suala la wenzi kuambatana kliniki si jambo la ajabu wala la aibu kwa
kuwa linaongeza uelewa na linasaidia kuijenga familia na jamii katika
suala zima la afya," alisema.
Mikoa mingine inayotajwa kuwa na maambukizi makubwa ya VVU ni pamoja
na Tabora,Kagera,Mwanza,Mbeya na Iringa
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment