*Ni wajawazito wa Hospitali ya wilaya ya Maswa
Na Samwel Mwanga-Maswa
TATIZO la kukatikatika kwa umeme linalowakabili wakazi wa wilaya ya
Maswa mkoa wa Simiyu juzi lilizua balaa katika hospitali ya wilaya
hiyo baada ya muunguzi katika wodi ya akinamama wajawazito kuzalisha
akinamama wawili gizani huku akitumia tochi ya simu aina ya Nokia
kutokanana kukosekana kwa nishati hiyo.
Tukio hilo lililotokea mwishoni mwa juma majira ya saa 1:00 usiku muda
mfupi baada ya umeme kukatika na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa
Akina mama hao ambao walikuwa wakipiga kelele za kuomba msaada kwani
muuguzi alikuwa mmoja katika wodi hiyo.
Watu walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa licha ya hospitali kuwa na
jenereta ambayo hutumika mara baada ya umeme kukatika lakini siku hiyo
haikuweza kuwasha kutokana na mhusika kutokuwepo eneo hilo.
Bi Ziada Khamis ambaye alishuhudia tukio hilo alisema kuwa alifika
hospitalini hapo kwa ajili ya kupima BP ambapo mashine iko katika wodi
ya akina mama wajawazito lakini ghafla umeme ulikatika lakini muuguzi
aliyemkuta alikuwa katika chumba cha akinamama kujifungulia.
Alisema kuwa wakati akiwa akisubiri kupata huduma hiyo mara ghafla
alisikia sauti za akina mama waliokuwemo ndani ya chumba hicho
wakiomba msaada ndipo alipomuuliza muuguzi ambaye alimwomba aje
amshikie simu yenye tochi ili aweze kuwasaidia akina mama kujifungua
kutokana na kukosekana kwa umeme.
"mie ndiye niliyeshuhudia tukio la huyo muuguzi kuzalisha gizani siku
ya jumamosi akitumia mwanga hafifu wa tochi ya simu aina ya Nokia na
alikuwa pekee yake kwani mwenzake alikwenda kuwaomba walinzi wawashe
jenereta lakini wakasema mhusika hayupo hivyo ikabidi nimsaidie
kushika tochi ili aweze kuzalisha"alisema Ziada Khamis.
Bi Ziada ambaye pia ni Diwani wa viti maalum(Chadema)katika
halmashauri ya wilaya hiyo alisema kuwa kitendo hicho kinawafanya
wauguzi katika hospitali hiyo kufanya kazi katika mazingira magumu
huku akitupia lawama uongozi wa hospitali ya wilaya ya Maswa.
'hapa ni lazima Mganga Mkuu awe makini sana vinginevyo hali hii
ikiendelea inaweza kusababisha vifo visivyotarajiwa kwa akina mama
wajawazito na watoto watakaojifungua nalikitokea jambo hilo
wanaolaumiwa ni wauuguzi walioko katika wodi lakini na wenyewe
wanafanya kazi kazi katika mazingira magumu"alisema kwa masikitiko.
Baadhi ya wauguzi ambao waliongea na Mwandishi wa habari hizi kwa
masharti ya kutotaka majina yao yaandikwe gazetini walilalamikia
uongozi wa hospitali hiyo kwani umeme unapokatika inachukua muda mrefu
kuwashwa kwa jenereta hivyo kuwafanya wafanye kazi katika mazingira
magumu.
"mie lawama nazitupa kwa uongozi wa hospitali hili suala
tumelilalamikia kwa muda mrefu sana na ndiyo maana siye tulio wengi
tunatumia simu zenye tochi maana ukiwa zamu ya usiku umeme ukikatika
ndiyo zinatusaidia kuwahudumia akinamama wenzetu hasa wanaojifungua
kwa nyakati hizo"alisema mmoja wao.
Waliendelea kueleza kuwa kuzalisha kwa kutumia tochi ya simu ni jambo
la hatari kwani kunaweza kumsababishia madhara mama mjamzito iwapo
simu hiyo ikamdondokea lakini hawawezi kuacha kuwasaidia kwa kukosa
umeme huku wakisisitiza kuwa Mungu ndiye anayewasaidia.
Akizungumzia malalamiko hayo Mganga Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk
Jonathan Budemu amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kueleza kuwa ameanza
kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuweka bajeti ya kununua mashine ya
kufua umeme ambayo itakuwa inajiunganisha pindi umeme unapokatika.
'tatizo hili lipo na hasa umeme unapokatikakatika mara kwa mara hivyo
tumekaa tumeona ili kulimaliza tatizo hili ni kununu jenereta ambavyo
itakuwa ni atomatic kwani umeme wa Tanesco ukikatika inajiwasha mara
moja na hata kama mgonjwa anapasuliwa kazi inaendelea kama
kawaida"alisema.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment