Katika
kukabiliana na tatizo la ukame wa mara kwa mara,Halmashauri ya Wilaya
ya Meatu mkoani Simiyu inakusudia kuanzisha miradi ya kilimo cha
umwagiliaji katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Kwa mujibu wa
taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri
hiyo ya wilaya,John Wanga katika kikao cha Baraza la madiwani lengo la
kuanzishwa kwa miradi hiyo ni kuwawezesha wakazi wa wilaya hiyo
kukabiliana na tatizo la uhaba wa chakula kila mwaka.
"Kutokana na
hali ya ukame wilaya imetambua njia pekee ya kuwa na uzalishaji wa
uhakika ni kuimarisha kilimo cha umwagiliaji. Mkazo umewekwa zaidi
katika maeneo yanayofaa kwa kilimo hiki, maeneo yote yana jumla ya hekta
2,145 yaliyopo katika vijiji vya Mwagwila, Usiulize, Mwakasumbi na
Tindabuligi," alieleza Wanga.
Wanga alisema hivi sasa halmashauri
yake tayari imeanza mchakato wa utekelezaji waskimu ya umwagiliaji
katika Kijiji cha Usiulize itakayokuwa na ukubwa wa hekta 245 ambapo
tayari andiko na michoro ya mradi huo vimeishakamilika na kinachosubiriwa ni fedha kiasi cha shilingi bilioni nne.
Akifafanua
Wanga alisema skimu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Mwagwila uliopo
katika Bonde la Mto Semu ina ukubwa wa hekta 150 ambapo
itakapokamilika ujenzi wake inatarajiwa wakulima wapatao 350 watanufaika na mradi huo.
Hata hivyo, alisema katika maeneo yote hayo kilimo hicho cha umwagiliaji kitatekelezwa na
wakulima
wadogo kwa kutumia pampu za kusukuma maji pamoja na ndoo na hivyo
kuwawezesha kulima kwa wingi mazao ya chakula, mbogamboga na matunda
ambayo yatawaongezea vipato vyao baada ya kuuza.
Ofisi yangu kwa
ushirikiano wa ofisi ya mkuu wa wilaya tutahakikisha wakulima wote
katika maeneo yenye skimu hizi wanazingatia masharti ya kilimo bora na
ili kuhakikisha panakuwepo mafanikio tumeunda timu za viongozi na
wataalamu wa kilimo zitakazosimamia utekelezaji kuanzia ngazi ya kata
hadi wilaya, alisema Wanga.
Katika hatua nyingine Wanga aliwaomba
madiwani wa halmashauri hiyo ya wilaya kuwahimiza wakulima katika kata
zao kuhakikisha wanapanda mazao yanayostahimili ukame kama vile uwele na
mtama ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa chakula mwakani kutokana
na hali ya hewa kuonesha huenda mvua za masika zisinyeshe kwa kipindi
kirefu.
Chanzo;Majara
0 comments:
Post a Comment