WANANCHI
wilayani Maswa, Simiyu, wamemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kumwondoa
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Hilda Lauwo, kwa
madai hana uwezo wa kuongoza halmashauri hiyo.
Wananchi wamefikia hatua hiyo kutokana na tuhuma mbalimbali
zinazomkabili zikiwemo za matumizi mabaya ya fedha za halmashauri,
matumizi mabaya ya madaraka na kauli chafu kwa wananchi na watumishi
walioko chini yake.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Maswa baadhi ya wananchi
walisema tangu ahamishiwe katika wilaya hiyo akitokea wilaya ya Ludewa
alikokataliwa na madiwani amekuwa ni mzigo.
Walieleza amekuwa akitumia vibaya madaraka yake kwa kuchota mamilioni
ya fedha za safari zikiwemo fedha za mafuta ya gari sambamba na posho
ya dereva, lakini haendi safari.
“Kwa kuonyesha alivyo mbadhirifu wa fedha za halmashauri Mei 27 mwaka
huu alichukua sh milioni 3 kwa ajili ya kuhudhuria kikao cha Lake
Victoria Region Local Authorities Cooperation(LVRLAC) kilichofanyika
jijini Kigali, Rwanda Mei 29, lakini hakuhudhuria kikao hicho baada ya
kuzuiwa na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu na hivi karibuni amechukua sh
milioni 2 kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo ya wiki mbili ya kompyuta kwa
wakuu wa idara jijini Mwanza lakini akaenda mjini Entebe, Uganda,
kuhudhuria kikao cha LVRLAC,” alisema mmoja wa watumishi wa halmashauri
hiyo.
Walieleza kuwa mkurugenzi huyo amekuwa na safari za mara kwa mara
huku ofisi yake akiacha kaimu ambaye hawezi kutekeleza majukumu kutokana
na kutokuwa na maamuzi ya kutosha huku akitumia gari la halmashauri SM
4135 Landcluser VX kubebea pumba za nguruwe kutoka Maswa hadi nyumbani
kwake wilayani Korogwe, Tanga.
Hata hivyo, walitoa lawama kwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo,
Stephen Dwese, kuwa amekuwa akimkumbatia licha ya malalamiko dhidi yake.
Akizungumzia malalamiko hayo kwa njia ya simu, mkurugenzi huyo
alisema safari anazozifanya mara kwa mara huwa zina baraka kutoka kwa
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na wanaolalamika wana chuki binafsi naye.
Hata hivyo alipotakiwa kutolea ufafanuzi wa tuhuma zingine
zinazomkabili alikata simu na alipotafutwa simu yake haikupatikana tena.
Chanzo;Tanzania Daima
1 comments:
kiukweli anatakiwa afukuzwe ili liwe onyo na fundisho kwa watu wengie wenye tabia na mwenendo kama wake
Post a Comment