Home » » Sare za polisi zampeleka jela miaka 24

Sare za polisi zampeleka jela miaka 24

MAHAKAMA ya wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, imemhukumu kwenda jela
miaka 24 mkazi wa Bariadi, Luteja Magembe, baada ya kupatikana na hatia
ya makosa matatu, likiwemo la kukutwa na sare za polisi kinyume cha sheria.
Pia mtuhumiwa huyo alikutwa na hatia ya kukutwa na silaha za uhalifu.
Awali Mwendesha Mashtaka, Samuel
Kilabuko, aliiambia Mahakama hiyo kuwa makosa hayo matatu ni kinyume
cha sheria.
Kilabuko alisema mtuhumiwa huyo alitenda makosa mawili ya kuvunja na
kuiba, huku akitumia sare za polisi na ana stahili kupatiwa adhabu kali ili liwe fundisho kwa
wengine wenye tabia ama wenye dhamira ya kufanya uhalifu huo.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu na hakimu aliyesikiliza kesi hiyo, Robert
Oguda, mtuhumiwa alipewa nafasi ya kujitetea ambapo aliomba mahakama
imuonee huruma kwa kuwa kuna watu wanaomtegemea.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya, Oguda
alisema ameridhishwa na ushahidi wa upande wa mashtaka na
kutoridhishwa na upande wa mtuhumiwa hivyo alimtia hatiani kwa
kosa la kwanza la kukutwa na sare za polisi kinyume cha sheria.
Katika kosa hilo, atatumikia miaka mitatu chini ya kifungu namba 257, kilichofanyiwa
marekebisho mwaka 2002.
Aidha kwa upande wa kosa la pili kuvunja na kuiba nalo amehukumiwa
miaka 7 chini ya kifungu cha sheria namba 265 kilichofanyiwa marekebisho mwaka
2002, huku kosa la tatu la kupatikana na silaha mbali mbali za
kubomolea nyumba nalo amehukumiwa miaka 14. 
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa