Home » » Wakulima wataka Chiza naye ang'oke

Wakulima wataka Chiza naye ang'oke

Sakata la kuenguliwa mawaziri wanne, limechukua sura mpya baada ya wakulima wa zao la pamba katika Mikoa ya Simiyu na Shinyanga, kumuomba Rais Jakaya Kikwete, amwajibishe Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti juzi, baadhi ya wakulima hao walipongeza uamuzi wa Rais Kikwete kuwawajibisha mawaziri hao na kusisitiza kuwa, Mhandisi Chiza naye anapaswa kuwajibishwa kutokana na kitendo chake cha kuruhusu matumizi ya mbegu za pamba zilizogoma kuota.
 Walisema kitendo cha Mhandisi Chiza, Wakuu wa mikoa na Wilaya katika mikoa inayolima zao hilo kupigia debe mbegu za pamba zilizosambazwa na Kampuni ya Quton ambazo zimeondolewa manyoya wakidai ndizo zenye ubora na baadaye kugoma kuota, hakistahili kufumbiwa macho.
Mmoja wa wakulima hao, Bw. Christopher Nhale ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwabusalu, Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, alisema ni muhimu Rais Kikwete akamchukulia hatua Mhandisi Chiza kwa kuzembea na kusababisha wakulima wengi kupata hasara akidai mbegu hizo zina ubora mkubwa.
"Binafsi nimepata hasara kubwa, nilipanda mbegu hizi katika shamba langu lenye ukubwa wa ekari 12, hakuna hata mbegu moja iliyoota na wakati napanda nilizingatia masharti yote ambayo niliambiwa, sijui kama Serikali itakuwa tayari kunifidia.
"Viongozi wetu akiwemo Mhandisi Chiza alizipigia debe mbegu hizi na kuna zingine zina ubora lakini matokeo yake yamekuwa tofauti...
Waziri alikurupuka kubariki matumizi ya mbegu hizi ikionesha hakufanya utafiti wa kina kama kweli zina ubora badala yake aliungana na wenzake kuzipongeza," alisema.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mwanhuzi, wilayani Meatu, Elia Shukia alisema hata kama Mhandisi Chiza atawajibishwa, bado Serikali inapaswa kuwalipa fidia wakulima wote waliopanda mbegu hizo na kugoma kuota hivyo wamelazimika kupanda mbegu nyingine upya zilizodaiwa hazina ubora.
N a y e Mw e n y e k i t i w a Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, mkoani humo, Justin Sheka alisema umefika wakati wa Serikali kuwathamini wakulima wa zao hilo badala ya kuwaacha kama watoto yatima wasio na walezi kutokana na usumbufu wanaoupata katika ulimaji wa pamba.
"Ni vizuri Serikali ikachukua uamuzi mgumu wa kuwasaidia wakulima wa pamba tofauti na ilivyo sasa, hawana mtu wa kuwasaidia na pale wanapopata matatizo hawalipwi fidia, wanunuzi wa pamba uchumi unapoyumba Serikali huwafidia hasara walizopata," alisema.
Katibu wa Umoja wa Wazee (UWAKA) wilayani Kahama, Bw. Paulo Ntelya, alisema mbali ya kuwajibishwa mawaziri hao, Rais Kikwete anapaswa kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji wote ndani ya Serikali ambao wamehusika kwa njia moja au nyingine kupigia debe mbegu za Quton na kusababisha wakulima wa pamba wapate hasara.
"Watendaji wetu ndani ya Serikali, wakuu wa Mikoa, Wilaya na Bodi ya Pamba walioshinikiza matumizi ya mbegu hizi bila kutoa nafasi ya majaribio, wanastahili kuchukuliwa hatua za kinidhamu," alisema Bw. Ntelya.
Hivi karibuni, wakulima wa zao hilo Wilaya za Kahama, Kishapu na Shinyanga, mkoani Simiyu na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora, walilalamikia mbegu za Quton kugoma kuota na kusababisha wapate hasara.
Awali, wakuu wa Wilaya ya Kahama, Nzega mkoani Tabora, Bukombe na Geita mkoani Geita pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, walihamasisha matumizi ya mbegu hizo na kuwapiga marufuku wakulima wasipande mbegu zenye manyoya hadi Rais Kikwete alipoingilia kati sakata hilo

Chanzo;Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa