MASHINDANO
ya Serengeti Marathon mwaka 2013, yamemalizika katika wilaya ya Busega,
mkoani Simiyu, na washindi kukabidhiwa zawadi zao, ikiwemo zawadi ya
juu ya shilingi milioni 2.5.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na mkurugenzi wa Serengeti Marathon,
ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Busega, na mwenyekiti wa chama cha
mapinduzi (CCM), mkoani Simiyu, Dk. Titus Kamani, yameshirikisha
wakimbiaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Akimkaribisha mkuu wa mkoa wa Simiyu, Paschal Mabiti kwa ajili ya kutoa
zawadi na kufunga mashindano hayo, Dk. Kamani amesema kuwa yalikuwa ya
mbio za kilomita 42, 21 na tano kwa wazee na kwamba yalianzia katika
hifadhi ya taifa ya Serengeti na kumalizikia katika eneo la Stop Over,
lililoko jirani na hifadhi hiyo katika kijiji cha Lukungu wilayani
Busega.
Amesema kuwa washiriki wa mashindano hayo walikuwa wametoka katika mikoa
ya Singida, Mwanza, Mara, Arusha, Kilimanjaro, Dar es salaam, Tabora na
wenyeji Simiyu, pamoja na wengine kutoka nchi za nje za Kenya, England
na Sweden na kwamba yalishirikisha wanaume kwa wanawake.
Amesema kuwa lengo la mashindano hayo ni kuhamasisha uhifadhi, kupiga
vita ujangili na kutangaza utalii, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni
kupig vita ujangili wa wanyama pori katika hifadhi zetu.
Akitoa zawadi kwa washindi mkuu wa mkoa wa Simiyu Mabiti, kwa niaba ya
waziri mkuu Mizengo Pinda, alimpongeza Dk. Kamani kwa kuanzisha
mashindsano hayo kwani yana lengo zuri la kulinda hifadhi na kutangaza
utalii.
Aidha, ameongeza kuwa pia mashindano hayo kwa namna moja pamoja na kuwa
ajira kwa washiriki, lakini pia yanadumisha ushirikiano, umoja na upendo
kwa washiriki ambao wanatoka maeneo mbalimbali wakiweo wageni kutoka
nje ya nchi na kwamba pia yanadumisha ushirikiano wa Afrika mashariki.
Mabiti amewataka washiriki wa mashindano hayo hasa waliotoka nje ya nchi
kuwa mabalozi katika nchi zao kwa kutangaza nchi yetu katika suala zima
la utalii na vivutio vilivyopo ambavyo ni vingi sana.
Aidha, amewataka wananchi wa wilaya ya Busega na mkoa wa Simiyu kwa
ujumla, mwakani kujitokeza kwa wingi kwenye mashindano hayo, ili waweze
kujinyakula zawadi.
Washindi katika mashindano hayo walikabidhiwa zawadi ya fedha tasilimu
kuanzia sh. 20,000 hadi shilingi milioni mbili na nusu, na medali za
fedha, ambapo wakimbiaji kutoka nchini ya Kenya walionekana kung’ara na
kukamata nafasi za juu, wakifuatiwa na wa mikoa ya Arusha na Manyara, na
pia wenyeji wa wilaya ya Busega waliibuka washindi na kukabidhiwa
zawadi.
Mashindano ya Serengeti Marathon yalianza rasmi mwaka jana na yamekuwa
yakifanyika kila mwanzoni mwa mwezi wa desemba katika wiki ya kwanza.
Wadhamini wa mashindano hayo mwaka huu walikuwa ni pamoja na Grumet Fund
Tanzania, Coca cola, WWF, Hifadhi za taifa (Tanapa), Serengeti
Breweries, NSSF, Hifadhi ya Serengeti na Board Of Trusrees.
Home »
» Mashindano ya Serengeti Marathon mwaka 2013 yamalizika, Wakenya watwaa zawadi za juu
0 comments:
Post a Comment