Home » » Wananchi Simiyu watakiwa kukomesha ujangili, mauaji ya Albino, Vikongwe

Wananchi Simiyu watakiwa kukomesha ujangili, mauaji ya Albino, Vikongwe

WANANCHI katika mkoa wa Simiyu, wametakiwa kushirikiana na serikali, ili kukomesha vitendo vya uhalifu, vikiwemo vya ujangili katika hifadhi za taifa na mauwaji ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) kwa imani za ushirikina pamoja na ukeketaji wa watoto wa kike. Mkuu wa mkoa wa Simiyu Bw. Paschal Mabiti, ametoa rai hiyo juzi katika eneo la Stop over, karibu na hifadhi ya taifa ya Serengeti, wakati akihutubia wananchi, baada ya kufunga mashindano ya Serengeti Marathon mwaka 2013. Bw. Mabiti aliyekuwa anamwakilisha waziri mkuu Mizengo Pinda, amesema kuwa kuna ujangili wa kutisha katika hifadhi za taifa, ambapo majangili yamekuwa yakiua wanyama mbalimbali wakiwemo Faru na Tembo, hali ambayo inahatarisha kutoweka kwa wanayama hao. Aidha, amesema kuwa ni jukumu wananchi wote mkoani hapa, kushirikiana na serikali ili kukomesha ujangili huo, pamoja na vitendo vingine vya uhalifu, hususan mauwaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Abino) pamoja na vikongwe kwa imani ya ushirikina. Amesema kuwa pia ni wajibu wa wananchi wote kupiga vita ukeketaji wa watoto wa kike kwani hali hiyo inahatarisha maisha yao. Amesema kuwa iwapo wananchi wote mkoani hapa wakishirikiana na serikali, katika kuhakikisha wanaimarisha uhifadhi, ikiwa ni pamoja na kuwataja bayana wanaoendesha vitendo hivyo,, hali hiyo inaweza kudhibitiwa na hifadhi zetu kuwa endelevu. Mbali na kuhifadhi hifadhi ya taifa ya Serengeti na maeneo tengefu, pia aliwataka wananchi kuhifadhi ziwa Victoria, ili liweze kuwa endelevu kwa kuacha uvuvi haramu ambao unahatarisha viumbe hai vya majini. Mapema mbunge wa jimbo la Busega, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoani Simiyu, Dk. Titus Kamani, aliyeandaa mashindano hayo kwa ajili ya kutangaza utalii na kuhamasisha uhifadhi endelevu, amesema kuwa vitendo vya uwindaji haramu vimekuwa vikisababisha kuharibu uchumi wa nchi. Dk. Kamani amesema kuwa iwapo hali hiyo haitadhibitiwa ipasvyo, upo uwezekano mkubwa wanayama kumalizika na hivyo kukosa fursa ya kupata watali ambao wamekuwa wakiingizia taifa fedha nyingi za kigeni. Amesema kuwa pia mauwaji ya Albino na vikongwe kwa imani za ushirikina na ukeketaji wa mtoto wa kike, ni vitendo ambavyo kwa kiasi kikubwa vinauchafua mkoa huo wa Simiyu, na hivyo kamwe haviwezi kuvumiliwa.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa