Home » » JK auzindua Mkoa wa Simiyu

JK auzindua Mkoa wa Simiyu

  Rais Jakaya Kikwete
Simiyu. Rais Jakaya Kikwete amezindua Mkoa mpya wa Simiyu na wilaya zake huku akisimikwa kuwa Mtemi wa Kisukuma na kupewa jina la MunguBhanu lenye maana ya Mungu watu.
  Katika uzinduzi  huo uliofanyika juzi jioni kwenye Uwanja wa Mashujaa wa Bariadi Mjini na kuahirishwa baada ya  mvua kunyesha, Rais alieleza kuwa lengo la Serikali katika uanzishaji mikoa hiyo na wilaya zake ni kusogeza huduma karibu na wananchi.
  Hata hivyo, sherehe hizo ziliendelea jana asubuhi ambapo Rais Kikwete alisimikwa kuwa Mtemi wa Kisukuma, shughuli zilizoambatana  na maombi ya kuomba baraka ya mvua, hekima, utajiri na neema kwa ushirikiano wa wazee wa jadi ambao ni watemi wa Kabila la Kisukuma mkoani humo.
Zoezi la kuuombea baraka Mkoa wa Simiyu pamoja na kuusimika kijadi, liliendeshwa na Watemi Charles Doto Itale wa Bujashi akiwa pamoja na Mtemi Andrew Chenge (Itilima) Mbunge wa Bariadi Mashariki, Wenseslaus Seni (Kanadi), John Ngemela (Magu) waliomvisha joho na kumkabidhi Utemi  Rais Kikwete.
Mkoa wa Simiyu ulianzishwa rasmi mwaka jana na kuwa mkoa wa nne kati ya mikoa iliyogawanywa katika maeneo mbalimbali ikiwamo mikoa ya  Geita, Njombe pamoja na Katavi hivyo kuifanya Kanda ya Ziwa kuwa na jumla ya mikoa sita.
Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia alieleza kuwa Serikali imetenga Sh17 bilioni kwa ajili ya mkoa huo fedha ambazo amedaiwa ni kwa ajili ya kujenga miundombinu pamoja na nyumba za watumishi hivyo alitoa wito wa matumizi yaliyokusudiwa.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa