WATUMISHI wanne wa
halmashauri ya wilaya ya Busega, mkoani Simiyu, waliokuwa wamefukuzwa kazi na
madiwani mwaka jana kutokana na tuhuma mbalimbali, ikiwemo ya ubadilifu wa
fedha za mahindi ya msaada, pamoja na kukamatwa na rushwa na Takukuru,
wamerudishwa kazini baada ya kukata rufaa.
Watumishi hao ambao
watatu ni maafisa watendaji wa vijiji na mmoja afisa mtendaji wa kata, jana
wamethibitishwa kurudishwa kazini kwenye kikao cha kwanza cha baraza la
madiwani wa halmashauri ya wilayaya Busega, kilichofanyika katika mji mdogo wa
Lamadi wilayani humo.
Mwenyekiti wa
halmashauri ya wilaya mpya ya Busega, Bw. John Lukale, amesema kuwa watendaji
wawili walikamatwa na takukuru kwa tuhuma ya kuomba rushwa na wengine
walikamatwa wakiwa wamefuja fedha za mahindi ya msaada yaliyotolewa serikali
kwa ajili ya kuuzia wananchi kwa bei nafuu.
Bw. Lukale amesema
kuwa kufuatia hali hiyo watumishi hao walifukuzwa kazi baada ya kubainika
kwamba wanayo makosa.
Amesema kuwa baadaye
watumishi hao walikata rufaa katika utumishi wa umma, na ikaamriwa warejeshwe
kazini na kwamba kwa jinsi hiyo, baraza la madiwani sasa limethibitishwa
kurejeshwa kazini.
Wakichangia hoja hiyo
madiwani hao wamesema kuwa pamoja na watendaji hao kurejeshwa kazini, ni vema
sasa wabadilishiwe vituo vya kazi kwa sababu wananchi wa maeneo husika hawana
imani nao tena, lakini pia hali hiyo ni kwa ajili ya usalama wao.
Kaimu mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Busega, Bw. Pamphil Masashua, amewataka
watendaji wote kufuata miiko na maadili ya kazi yao, vinginevyo hatua za
kinidhamu na kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Katika kikao hicho
mkuu wa wilaya ya Busega, Bw. Paul Mzindakaya, amewataka madiwani na
watendaji wote wa serikali wilayani humo kushirikiana na kuwa kitu kimoja, ili
kuharakisha maendeleo katika wilaya hiyo mpya.
0 comments:
Post a Comment