Mkuu wa wilaya ya Maswa, mkoa wa Simiyu, Luteni
mstaafu, Abdalah Kihato, amewaagiza viongozi wote wilayani humo kuhakikisha
kuwa wananchi wanafuata kanuni za usafi wa mazingira ili kutimiza malengo ya
kuuweka mji huo katika hali ya usafi.
Hayo yalibainishwa jana mjini Maswa wakati
akifungua kikao maalum cha wadau wa usafi wa mazingira wilayani humo
kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo na kuwashikirikisha
viongozi mbalimbali.
Alisema mji wa Maswa ni miongoni mwa miji ambayo
imekithiri kwa uchafu, hivyo ni vizuri wakaanzisha siku maalumu ya usafi wa
mazingira kila juma.
“Mji wetu kwa kweli ni miongoni mwa miji ambayo
imekithiri kwa uchafu, hivyo ni vizuri tukaanzisha siku maalum ya kufanya usafi
wa mazingira, kila juma tutaanza katika mji wa Maswa na baadaye zoezi hili
litaendelea wilaya nzima,” alisema.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia
70 ya magonjwa yanayotibiwa katika vituo vya afya nchini, yanahusiana na
uchafuzi wa maji na mazingira.
Aliyataja madhara mengine kuwa ni pamoja na
kuathiri mandhari ya makaazi ya watu kutokana na kuzagaa hovyo kwa uchafu wa
kila aina ukiwemo taka ngumu kama mifuko ya plastiki, harufu mbaya inayotokana
na kuoza kwa taka na maji machafu yanayotiririka hovyo.
Hata hivyo alisema ili suala la usafi wa mazingira
liweze kudumu ni bora sasa sheria ya usafi wa mazingira ikaweka msisitizo kwa
ulipaji wa faini ya papo kwa hapo kwa kila mkazi anayekamatwa akitupa uchafu
katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Pia alitumia nafasi hiyo kuwaonya viongozi wa
kisiasa kuacha kutumia nyadhifa zao kuingilia kazi ya usafi wa mazingira kwani
kufanya hivyo ni kuwarudisha wananchi nyuma kimaendeleo.
Naye ofisa mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa
Maswa, Rogers Lyimo, alisema kutokana na ongezeko la kasi la watu katika mji
huo sambamba na ukuaji wa sekta binafsi hasa maeneo ya kibiashara, kwa sasa mji
huo umekuwa ukizalisha zaidi ya tani 15 kila siku za uchafu.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment