Home » » Migogoro ya ardhi yachangia mauaji ya vikongwe

Migogoro ya ardhi yachangia mauaji ya vikongwe

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema mauaji ya vikongwe katika mikoa ya Kanda ya Ziwa sasa hayasababishwi na imani za kishirikina tu, bali pia migogoro ya ardhi, mali na mirathi ndani ya jamii ya wafugaji na wakulima.
Kwamba, tatizo la ukiukwaji wa haki za binadamu, hasa elimu duni ndani ya jamii ya kifugaji na wakulima wa jamii ya Kisukuma, ni moja ya chanzo kikuu cha mauaji ya vikongwe katika mikoa ya Simiyu na Shinyanga.
Mauaji hayo sasa hayawakumbi vikongwe pekee bali hata kwa wanawake wenye umri mdogo.
Hayo yameelezwa jana na wakili wa LHRC, Shilinde Ngalula, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Maswa kuhusu kituo hicho kinavyotoa msaada wa sheria kwa watu wenye matatizo mbalimbali ya kisheria mkoani hapa.
Alisema lipo tatizo la uelewa wa utoaji wa haki kwa kutumia mabaraza ya ukoo, wazee na jamii maarufu kama Ndagashida chini ya wazee wa koo za kichifu na zile zilizowahi kuwa za kitemi na walinzi wa jadi (sungusungu) na kupuuza vyombo na taasisi za kutoa haki kama vile mahakama na mabaraza ya kata yaliyopo kisheria.
Alifafanua kuwa hatua hiyo imesababisha kutolewa kwa uamuzi wenye upendeleo unaochochea mauaji ndani ya jamii hiyo.
Ngalula alisema tatizo la elimu ya uraia na vitendo vya rushwa ndani ya taasisi hizo linasababishwa na ukosefu wa elimu ya kutosha, hasa juu ya haki za binadamu.
Kwamba hatua hiyo imeisababisha jamii hiyo kuamini masuala ya kishirikina na kuwepo migogoro ya mirathi, ardhi na mali ikiwemo mifugo na kusababisha mauaji hata kwa wanawake wenye umri mdogo kwa sababu ya kulipa kisasi.
Ngalula alisema kuwa mila kandamizi na desturi, mfumo dume ndani ya jamii, hasa za kifugaji kutomruhusu mtoto wa kike kumiliki ardhi, mali, kushiriki katika maamuzi, kunyanyaswa kijinsia na hata kupigwa na kukoseshwa elimu kwa makusudi pia ni tatizo.
Alifafanua kuwa mfumo wa maisha ya jamii ya wafugaji na wakulima ndani ya mikoa hiyo, hususani Simiyu na Shinyanga kwa tabia ya wakuu wa kaya hasa wanaume kuhamahama na mifugo na familia zao, imekuwa ikiwakosesha haki ya msingi ya mtoto kupata elimu na makuzi bora.
Alifafanua kuwa badala yake wamekuwa wakilazimishwa kuchunga mifugo na kusababisha kuwa na kundi kubwa la watu wasio na elimu na kuwepo uvunjwaji mkubwa wa sheria na haki za binadamu ndani ya jamii hizo.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa