VIJANA katika wilaya ya Busega,
mkoani Simiyu, wametakiwa kuchangamkia fursa zinazojitokeza kwenye maeneo yao,
ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini.
Ushauri huo umetolewa jana na
mwenyekiti wa wilaya mpya ya Busega, Bw. Lukale John Charles, katika mji mdogo
wa Lamadi, wilayani Busega wakati akifungua semina ya kuwapa uwezo vijana ili
waweze kujua wajibu wao kama vijana, elimu ya ujasiriamali, kujua sera ya
vijana, uongozi na stadi za maisha.
Bw. Charles amesema kuwa vijana ni
nguzo ya taifa hivyo wanafaa kuwezeshwa, ikiwa ni pamoja na kuchangamkia fursa
zinazojitokeza ili waweze kuondokana na umasikini.
Amesema kuwa vijana wanazo fursa
nyingi lakini wamekuwa wakishindwa kuzitumia fursa hizo, na badala yake
kusingizia serikali kwamba haijawafanyia chochote.
Aidha amewahimiza vijana kukazania
elimu kwani njia pekee ya kujiondoa kwenye lindi la umasikini ni elimu, ambayo
ndio msingi wa maisha.
Amesema kuwa kwa sasa serikali
kupitia wizara ya habari, utamaduni, vijana na michezo, imetenga kiasi cha
shilingi bilioni 6.1 ambazo zitawekwa kwenye saccos za vijana za wilaya husika
na kwamba ni vema sasa vijana wakachangamkia hiyo fursa kwa kuanzisha benki
hiyo na kujiunga kwenhe vikundi ili waweze kupata mkopo wa fedha hizo.
Awali mkurugenzi mtendaji kutoka
wizara ya habari, utamaduni, vijana na michezo, Dk. Kisusi Stevin Kisusi,
amesema kuwa vijana ni muhimu sana katika jamii na taifa kwa ujumla, hivyo ni
vema wakaijua sera yao, badala ya kukalia kulalamika kwamba serikali bado
haijawafanyia chochote.
Bw. Kisusi amesema kuwa vijana ambao
ni milioni 16.2 wakiwemo wanawake milioni 6.3 na wanaume milioni 7.9 sawa
na asilimia 35 ya watu wote na asilimia 68 ya nguvu kazi ya taifa, inapaswa
waisome na kuijua sera yao, juu ya wajibu wao na serikali kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment