na Samwel Mwanga, Simiyu
KUSUASUA kwa
ununuzi wa Pamba wilayani Maswa Mkoa mpya wa Simiyu kumewasikitisha viongozi wa
wilaya hiyo licha ya kuwepo kwa kampuni 10 zilizoidhinishwa na Bodi ya Pamba
(TCB) kufanya kazi hiyo msimu huu.
Masikitiko hayo
yalioneshwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Luteni msataafu Abdallah Kihato na
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hilda Lauwo, wakati wa kikao maalumu cha
kuhakikisha pamba yote wilayani humo imenunuliwa kabla ya mvua za vuli.
Katika hali ya
kushangaza wakuu hao wamedai kusikitishwa na kasi ndogo ya makampuni yaliyopewa
vibali vya kununua zao hilo kuwakopa wakulima na kukwepa ushuru wa halmashauri
hiyo wa asilimia mbili badala ya asilimia tano kwa mujibu wa agizo la serikali.
Agizo hilo la
serikali limetokana na kudorora kwa biashara ya pamba kwenye soko la dunia.
Luteni Kihato
alisema licha ya wakulima kukubali kuuza pamba yao kwa sh 660 bado kampuni hizo
zimeshindwa kuinunua na kujikuta wakimkopa mkulima na kusababisha malalamiko
kutoka kwa wakulima.
Kwa upande wake
mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo alisema amechanganyikiwa, hasa
akizingatia maelekezo anayopewa na madiwani kukusanya ushuru na kufikia malengo
yaliyowekwa, huku wanunuzi hao wakikwepa kulipa hata ushuru wa asilimia mbili.
Miongoni mwa
wajumbe waliokuwemo kwenye kikao hicho ni Mbunge wa Maswa Mashariki, Slyvester
Kasulumbayi, Katibu wa Mbunge wa Maswa Magharibi, Ziadah Hamisi, Mwenyekiti wa
Halmashauri hiyo Steven Dwese, Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi wa Bodi ya
Pamba Tanzania, James Shimbe na Mkurugenzi wa Bodi hiyo Kanda ya Ziwa, Jones
Bwahama.
Wilaya ya Maswa
inatarajia kununua kiasi cha kilo milioni 35,000 za pamba msimu huu na
kujipatia zaidi ya shilingi bilioni 1.7 za ushuru wa pamba mbegu,
ikilinganishwa na zaidi ya kilo 8,000,000 zilizonunuliwa msimu uliopita
2011/12.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment