Home » » MASWA WAISUBIRI M4C KWA HAMU

MASWA WAISUBIRI M4C KWA HAMU



na Samwel Mwanga, Maswa
WANANCHI wa Wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu, wanasubiri kwa hamu vuguvugu la mabadiliko linalofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), maarufu kwa jina la M4C, ili kurudisha kadi za Chama Cha Mapinduzi(CCM) na kukizika chama hicho wilayani humo.
Wakizungumza na Tanzania Daima mjini Maswa jana, wakazi hao walisema wamechoshwa na tabia ya viongozi wa CCM wilayani humo kutotaka mabadiliko huku hawakubaliki katika jamii hali ambayo imewafanya wananchi kupoteza imani na chama hicho.
“Sasa binadamu amefikia kikomo cha uvumulivu, viongozi ndani ya CCM wilayani Maswa hawataki mabadiliko kazi yao ni kung’ang’ania madaraka hebu angalia viongozi waliokisambaratisha chama ndiyo hao hao wamerudi kushika nyadhifa kwa kutumia nguvu ya fedha na hawakubaliki ndani ya jamiii,”alisema Masele Mhoja.
Wananchi hao kutoka katika kata mbalimbali za wilaya hiyo walisema uchaguzi uliomalizika ndani ya chama hicho ndiyo umechimba shimo la kukizika kutokana na viongozi waliochaguliwa kuwa vinara wa chuki na fitina.
“Huu uchaguzi tuliomaliza ndani ya chama ndilo shimo la kukizika chama chetu, kwani hao viongozi wa ngazi za juu nani asiyewafahamu ndiyo mabingwa wa chuki na fitina hawataki chama kiwe na mabadiliko ya wasomi ukiwa msomi katika CCM Maswa wewe ni adui. Kweli tutafika?”alihoji Kada mmoja wa chama hicho, Jishuli Jidayi.
Wamesema wamechoshwa na tabia ya viongozi hao ambao katika uchaguzi uliopita walisababisha majimbo yote ya Maswa Mashariki na Maswa Magharibi kuchukuliwa na CHADEMA huku wakipoteza Kata tano zilizokuwa chini yao ambao wamegeuzwa kama kipaza sauti cha mafisadi.
Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Maswa, Luhende Mipawa, alisema lengo ni kuifanya CCM kuwa chama cha upinzani na kwa kuanzia watahakikisha mamlaka ya mji mdogo wa Maswa inaongozwa na chama hicho.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa