na Samwel Mwanga, Maswa
UPEPO
mkali uliozuka ghafla katika uwanja wa Nguzo Nane ulioko wilayani Maswa, Simiyu
wakati wa sherehe za mapokezi ya Mwenge wa Uhuru umesababisha watu kadhaa
kujeruhiwa wakiwemo wanafunzi baada ya mahema yaliyokuwepo eneo hilo kuezuliwa.
Tukio
hilo lilitokea juzi, majira ya saa 10:45 jioni wakati wa risala ya utii ya
wananchi wa Wilaya ya Maswa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ikisomwa na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Danford Peter.
Wakati
risala hiyo ikisomwa, ghafla upepo mkali maarufu kwa jina la kimbunga ulitokea
na kuezua mahema yaliyokuwepo huku vyuma vikiwaangukia baadhi ya watu na
kuwasababishia majeraha.
Waliojeruhiwa
katika tukio hilo ni Pastory Elias (16), aliyejeruhiwa kichwani na mkono wa
kulia, Justine Abdu (12) aliyejeruhiwa mkono wa kulia, Chausiku Selemani (14)
aliyejeruhiwa mkono wa kushoto na mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Juma
aliyejeruhiwa mkono wa kushoto wote wakiwa ni wanafunzi wa shule za msingi
walioalikwa kwenye sherehe hiyo.
Wengine
ni Juma Hassan (26) aliyejeruhiwa sehemu ya shingoni na mkono wa kushoto na
Edward Salvatory (45) aliyejeruhiwa sehemu ya bega lake la kulia na kuchomwa na
kitu chenye ncha kali.
Kutokana
na tukio hilo, hotuba hiyo ilisitishwa kusomwa kwa muda huku Kiongozi wa mbio
za Mwenge, Luteni Honest Mwanosya, akiwa makini kuhakikisha Mwenge huo haupati
madhara yoyote ikiwemo kuzimika.
Jumla
ya miradi yenye gharama ya sh bilioni 3.6 ilizinduliwa katika sherehe hizo,
ikiwamo ya elimu, afya, maji, maliasili na mazingira.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment