na Samwel Mwanga, Simiyu
HALMASHAURI ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imeanza kubaini vyeti halisi vya walimu wote wa shule za sekondari na msingi ili kujiridhisha juu ya ajira zao.
Halmashauri hiyo imeajiri walimu 2,030 kati yao 1,600 wanafundisha kwenye shule za msingi na wengine 430 wanafanya kazi shule za sekondari. Idadi hiyo haihusishi walimu walioajiriwa mwaka wa fedha 2011/2012.
Utambuzi huo ulianza mwishoni mwa mwezi uliopita ambapo wakaguzi wa elimu wanahakiki vyeti vya kuhitimu elimu ya sekondari, juu sambamba na vile vya kitaaluma kwa walimu wote.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Samwel Simbilla, alilieleza Tanzania Daima kwamba zoezi hilo litaisaidia kubaini uhalali wa vyeti vya walimu hao na kuwathibitisha hasa wenye kasoro kwenye ajira zao.
Alisema baadhi ya walimu wapo kazini lakini hawajathibitishwa, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu na sheria za ajira serikalini zinazomtaka mtumishi kuthibitishwa ndani ya miezi 12 baada ya kuanza kazi.
“Wapo walimu hapa Maswa wamefanya kazi zaidi ya mwaka mmoja lakini hawajathibitishwa hivyo kupoteza haki zao, kwa vile wanahesabika kuwa vibarua,” alisema kaimu na kuongeza kwamba kazi hiyo itafikia ukomo Septemba 8 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Simbilla, wamebaini kuwepo kwa walimu wasio na vyeti halali, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi.
Naye Ofisa Elimu ya Sekondari wilayani hapa, Paulina Ntagaye, alisema tayari zoezi hilo limekamilika kwa walimu wote wa sekondari ambao wanawake ni 92 na wanaume 338, bila kutaja idadi ya walimu waliokutwa na vyeti vya kughushi.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment