Home » » JANGWA LAINYEMELEA SIMIYU, SHIRIKA LAANZA KUPANDA MITI KUNUSURU HALI HIYO.

JANGWA LAINYEMELEA SIMIYU, SHIRIKA LAANZA KUPANDA MITI KUNUSURU HALI HIYO.

Mwandishi wetu, Busega-Simiyu Yetu

SHIRIKA la The East African Community Organisation (ECOVIC) limeanza mkakati wa kupanda miti katika wilaya ya Busega, mkoani Simiyu, ikiwa ni jitihada za kukabiliana na jangwa ambalo limeanza kujitokeza wilayani humo kutokana na wananchi kukata miti hovyo na kuharibu mazingira.

Mratibu wa shirika hilo, Bw. Jackison Ndobeji, ametoa tarifa hiyo jana kwa mbunge wa jimbo la Busega, Dk. Titus Kamani, alipotembelea eneo hilo, ikiwa ni ziara yake ya kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo jimboni humo.

Bw. Ndoboje amesema kuwa wameanza kupatanda miti wilayani humo wakianzia katika kijiji cha Mwabayanda, ambapo wamepanda jumla ya miche 50,000 na kwamba watapanda miti katika awamu tatu wilayani humo.

Amesema kuwa lengo la shirika hilo ni kupanda jumla ya miche 150,000 katika awamu tatu, ikiwa ni kwa kila mwaka kupanda miche 50,000 ambapo zoezi hilo limeanzia kwenye kitongoji cha Mwabayanda, pamoja na kwenye shule mpya ya msingi Lamboni inayojengwa kwa nguvu za wananchi.

Amesema kuwa shirika hilo limeamua kuanzisha mkakati huo wa upandaji miti, baada ya kufanya utafiti wa kina na kugundua kuwa eneo hilo linakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwa jangwa, kutokana na kushamiri kwa ukataji wa miti uliofanyika miaka ya nyuma na kuliacha eneo hilo likiwa halina miti kabisa.

Aidha, amesema kuwa shirika hilo linapanda miche ya miti aina ya mihale, ambayo inasambaa kwa haraka zaidi, ili kulinusuru eneo hilo lisigeuke kuwa jangwa.

Aliongeza kuwa miche hiyo imekuwa ikioteshwa na Shirika hilo, kupitia vikundi vyake vidogovidogo na kwamba kila mche mmoja thamani yake ni sh. 200.

Kwa upande wake Dk. Kamani amelipongeza shirika hilo kwa kuanzisha mkakati huo na kuwataka wananchi kuitunza na kuihifadhi miti inayopandwa, ili iweze kukua na kuleta manufaa kwa jamii.

Amesema kuwa miti hiyo itkikua italeta hewa safi kijijini hapo, ikiwa ni pamoja na kuzuia mmomonyoko wa ardhi, pamoja na kurudisha uoto wa asili ambao umekaribia kuisha kabisa katika eneo hilo.

Dk. Kamani pia aliwataka wananchi jimboni humo kujenga tabia ya kupanda miti na kuacha tabia ya kuharibu mazingira, kwani hali hiyo husababisha madhara makubwa ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Shirika la ECOVIC lina makao yake makuu hapa nchini katika mkoa wa Mwanza na linashughulika na mashirika madogo madogo yasiyokuwa ya kiserikali ya nchi tatu za Tanzania, Uganda na Kenya.

Blogzamikoa

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa