Home » » CHADEMA YAITESA CCM

CHADEMA YAITESA CCM

na Samwel Mwanga, Maswa
KATIKA kuonesha hali ya kuzidiwa na nguvu ya upinzani, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu kimewataka wanachama wake kuchagua viongozi wanaokubalika kwa wananchi.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho aliyemaliza muda wake wilayani humo, Sitta Mashala wakati akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa jumuiya hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya.
Alisema chama hicho kilifanya vibaya katika Uchaguzi Mkuu uliopita na kukosa majimbo yote ya Maswa Mashariki na Maswa Magharibi yaliyochukuliwa na CHADEMA kutokana na uongozi mbovu uliokuwepo ndani ya CCM wilayani hapa.
“Uchaguzi Mkuu uliopita wote mnajua hatukufanya vizuri, majimbo yote mawili ya uchaguzi katika viti vya ubunge yalichukuliwa na upinzani kutokana na udhaifu wa uongozi uliopita kwani walishindwa hata kutambua mchango wa viongozi waliopita wakaendekeza urafiki,” alisema.
Alisema viongozi hao waligeuza chama kama mali yao binafsi kufikia hatua ya kutorudisha majina ya wagombea waliokuwa na sifa na kinyume chake walirejesha majina ya wagombea ambao hawakubaliki kwa wananchi hali ambayo iliwafanya washindwe vibaya na wapinzani kuibuka washindi.
“Mnajua majina mengine ya viongozi wazuri hayakurejeshwa wakati wa uchaguzi ndani ya chama hata katika nafasi za uwakilishi. Mfano Mzee Charles Bukoye aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya alikuwa kiongozi safi, lakini akafanyiwa fitina jina halikurudi, akahamia CHADEMA,” alisema Mashala huku akishangiliwa na wajumbe.
Alisema kwa sasa CCM imepoteza mwelekeo kwa wananchi, hivyo ni vizuri wakachagua viongozi wanaoweza kurudisha matumaini hasa katika wilaya hiyo ambayo imekuwa ikipambana na upinzani kutokana na udhaifu wa uongozi uliopita.
Naye mwasisi wa CCM wilayani hapa, Kulwa Nangale, alisema viongozi walioko wanapaswa wasichaguliwe kwani hao ndio wamekifikisha chama hicho mahali kilipo sasa kutokana na kuoneana aibu.
Chanzo: Tanzania Daima

1 comments:

Simiyu press blog said...

HUO NDIYO UKWELI YUPO MKT WA CCM WILAYA YA MASWA,PETER BUNYONGOLI NA KATIBU MWENEZI WA CCM WILANI HUMO,JEREMIAH SHIGALA AU MAKONDEKO NDIYO WANAOKIHARIBU CHAMA HICHO WILAYANI MASWA.

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa